Na: Beatus Maganja, Dar es Salaam.
MAMLAKA ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) inatumia maonesho ya 47 ya kimataifa ya kibiashara yanayoendelea Jijini Dar es Salaam kuhamasisha Umma wa watanzania wawekezaji na wageni kutoka mataifa mbalimbali kuwekeza katika maeneo inayoyasimamia huku ikijinasibu kuwa na fursa lukuki za uwekezaji
Akiongea na wageni waliotembelea banda la TAWA lililopo ndani ya banda la Wizara ya Maliasili na Utalii Afisa Mhifadhi Gregory Kalokole amesema TAWA ina uwanda mpana wa fursa za uwekezaji unaotoa mwanya kwa wawekezaji wa aina mbalimbali kuwekeza katika taasisi hiyo
Akizitaja fursa hizo Kalokole amesema yapo maeneo mengi yanayohitaji wawekezaji na uwekezaji katika taasisi hiyo kama vile maeneo ya utalii wa picha kwenye maeneo ya hifadhi za Wanyamapori, maeneo ya kihistoria yenye Utalii wa kiutamaduni, eneo la uwekezaji mahiri (Special Wildlife Investment Concession Areas – SWICA), Uwindaji wa Kitalii na Ufugaji wa Wanyamapori.
“TAWA imetenga maeneo kadhaa Kwa ajili ya kufanyika shughuli za utalii wa picha kutokana na ikolojia na aina ya vivutio vilivyopo katika maeneo hayo ikiwemo Pori la Akiba Mpanga/Kipengere eneo ambalo lina maporomoko ya maji zaidi ya 10 ambayo hutoa burudani safi Kwa watalii” amesema Kalokole.
“Mapori mengine ya Akiba ni Pande, Wamimbiki, Swagaswaga na Kijereshi ambapo wananchi wanakaribishwa kuwekeza kwenye miundombinu ya Utalii ikiwemo kujenga Kambi za Kulala wageni, hosteli, loji na maeneo ya mapumziko mafupi (Picnic Sites) ameongeza
Kwa Upande wake Afisa Habari wa TAWA Beatus Maganja ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wananchi Wote kutembelea banda la TAWA Ili kupata maelezo ya fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo katika taasisi hiyo.
“Hii ni fursa adhimu Kwa wawekezaji wote kutembelea banda letu ili waweze kupata ufafanuzi wa fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo katika taasisi yetu kwani TAWA ni sehemu sahihi Kwa uwekezaji na wawekezaji “ amesema
Maonesho haya yenye Kauli Mbiu “Tanzania ni Mahali Salama Pa Biashara na Uwekezaji” yameanza 28 Juni, 2023 na yanatarajiwa kufikia tamati 13 Julai, 2023.