Dar es Salaam. Juni 09, 2023.
Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imetangaza kuingia makubaliano na WIzara ya Elimu, Sayansi na Teknalojia kwa ajili ya kutoa ufadhili wa masomo ya ufundi kwa vijana wa Kitanzania.
Katika makubaliano hayo, NBC itaanza kutoa udhamini wa masomo mwaka huu 2022 na imetenga jumla ya shilingi milioni 100.
Wanufaika wa programu watakuwa ni vijana wa Kitanzania wenye umri kuanzia miaka 18 na kuendelea na ambao wanatoka katika familia zenye vipato duni. Programu itasimamiwa na Wizara Elimu, Sayansi na Teknalojia na Mamlaka ya Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) wataitekeleza.
Ufadhili huo wa masomo unaojulikana kama NBC Wajibika Scholarship, unalenga kuwapatia vijana ujuzi katika fani mbali mbali ikiwa ni jitihada za kuwafanya waweze kujiajiri na kuajiriwa. Mafunzo yatakuwa yakitolewa na Mamlaka ya Ufundi Stadi (VETA).
Akiongea wakati ya hafla ya makubaliano hayo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknalojia Profesa Adolf Mkenda alisema tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana linaweza kutatuliwa kwa kuwasaidia vijana kupata ujuzi ambao utawawezesha kujiajiri.
“Watanzania wengi wana umri kati ya miaka 15 na 45 na Serikali peke yake haiwezi kuwapatia ajira wote. Hata hivyo, kama kundi hili linapatiwa ujuzi sahihi wa kiufundi wanaweza kujiajiri wenyewe na kuwaajiri vijana wengine,” alisema.
Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa NBC Theobald Sabi alisema Benki hiyo inaendelea kuwekeza kwa jamii. “Tunayofuraha kuwa ushirikianio wetu huu na Serikali kupitia wizara ya elimu utawezesha vijana 1,000 kupata mafunzo ya ufundi na hivyo kuweza kujiajiri”
Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa, NBC inajivunia kupata fursa ya kuwawezesha vijana wa Kitanzania na kuwapa nafasi ya kutimiza ndoto zao. “Tunawajibu wa pamoja wa kuhakisha tunaliingiza kundi hili kubwa kwenye soko la ajira na kwa msingi huo benki ya NBC inafurahia kuanzisha programu ya ufadhili wa masomo maarufu kama Wajibika Scholarship ambayo itatoa mafunzo ya muda mfupi na kuwapatia vijana ujuzi utakaowasidia kujiajiri,” alisema.
Sabi alifafanua kuwa wanufaika pia watafaidika na programu mbali mbali za benki hiyo zitazowasaidia kukua ikiwa ni pamoja na, NBC Kuanasi, Klabu za kibiashara za NBC, ushauri wa kifedha, mikopo na kuunganishwa na masoko.
Mkurugenzi huyo pia alitumia nafasi hiyo kumweleza waziri kuwa NBC imeanzisha akaunti maalum kwa ajili ya waalimu inayojulikana kama “Akaunti ya Mwalimu” ambayo imebuniwa mahsusi kwa ajili ya waalimu.
“Ninayo furaha kuwataarifu walimu wote kuwa tumekuja na akaunti maalumu kwa ajili yao ambayo inazingatia mahitaji yao ya huduma za kifedha. Akaunti hii haina makato ya mwezi na pia gharama za kufanya miamala ni ndogo sana. Pia inakuja ikiwa na bima na kutoa fidia inapotokea mteja anapata ulemavu au kufariki. Nawasihi waalimu wote wafike katika matawi yetu yaliyo jirani nao kwa ajili ya kupata taarifa zaidi,” alisema
MWISHO.