Na: Mwandishi wetu, IRINGA.
Katibu mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo amemtaka mkandarasi anayejenga Uwanja wa Ndege wa Nduli Mkoani Iringa ahakikishe kuwa unakamilika ifikapo Agosti mwaka huu, huku akitoa Rai kwa Wananchi Mkoani humo kuhakikisha wanautumia vizuri Uwanja huo, ili waweze kunufaika na fursa ya uwepo wake kwa Kujiimarisha Kiuchumi kupitia Sekta ya Kilimo na Utalii kwenye Ukanda huo.
Komredi Chongolo ametoa rai hiyo leo Juni Mosi, 2023, baada ya kukagua mradi wa upanuzi Uwanja wa Ndege Nduli, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku saba ya kukagua uhai wa CCM, Utekelezaji ilani ya uchaguzi ya Chama hicho ya 2020-2023 pamoja na Kuzungumza na Makundi mbalimbali ya Kijamii.
“Uamuzi wa Serikali kuujenga upya uwanja wa ndege wa Nduli, dhamira yake kubwa ni kuanza kufungua fursa kwa wananchi wa mikoa ya kusini kuweza kusafirisha bidhaa na Biashara mbalimbali zinazotokana na Sekta ya Kilimo.
Pia amesema Wananchi wa Kanda ya Kusini wanatarajia kunufaika kupitia Sekta ya Utalii baada ya Uwanja wa Ndege wa Nduli Kukamilika, ambapo fursa ya ujio wa Wageni kutembelea vivutio vya Utalii itakuwepo ambapo wananchi watapata fedha na Serikali itaongeza mapato.
Katika hatua nyingine katibu mkuu huyo wa CCM komredi Chongolo amewakumbusha Wakazi wa Iringa kuendelea kutunza utamaduni wa mkoa huo ili wageni wanaoingia wajue na Kujifunza tamaduni za mikoa ya Kusini mwa Tanzania.
Katibu Mkuu komredi Daniel Chongolo katika ziara yake hiyo ameambatana na Katibu wa NEC itikadi na Uenezi Sophia Mjema pamoja na Katibu wa NEC Oganaizesheni Issa Haji Gavu.