Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Prof. Raphael Chibunda akizungumza katika Maonesho ya 17 ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania yaliyokuwa yakiendelea katika Viwanja vya Mnazi Mmoja alipokuwa akitoa neno la shukrani kabla ya kuhitimisha rasmi hafla ya kufungwa rasmi Maonesho ya 17 ya Vyuo Vikuu Jijini Dar es Salaaim.
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Dkt. Francis Michael (wa tatu kushoto) akimsikiliza Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Profesa Raphael Chibunda, alipokuwa akitoa maelezo Juu ya Maabara ya kisasa inayotembea inayotumika kupimia sampuli mbalimbali za Wanyama, Mimea na Binadamu kwenye Maonesho hayo Jijini Dar es Salaam. (wa pili Julia) ni, Katibu Mtendaji wa TCU Prof. Charles Kihampa.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu Dkt Francis Michael akiangalia Nguo zilizobuniwa na kishonwa na wanafunzi wajasiriamali kutoka SUA. (PICHA NA: HUGHES DUGILO)
Na: Hughes Dugilo, DAR
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Profesa Raphael Chibunda amesema kuwa uwepo wa Maonesho ya Taasisi za Elimu ya Juu kunaongeza wigo wa Taasisi hizo kuweza kujitangaza na kwamba wanafunzi wanapata fursa ya kukutana na Vyuo Vikuu moja kwa moja na kufanya udahili.
Aidha amehimiza uwepo wa maonesho hayo kila mwaka huku akiipongeza Wizara ya Elimu kupitia Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kwa kuwezesha kufanyika kwa Maonesho hayo kwa mafaniko makubwa.
Profesa Chibunda ameyasema hayo wakati alipokuwa akitoa neno la shukrani katika hafla ya kufunga rasmi Maonesho hayo Julai 23, 2022 yaliyofanyika kwa siku sita katika viwanja vya Mnazi mmoja Jijini Dar es Salaam ambapo Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu vilishiriki.
Awali mapema katika ziara yake ya kutembelea mabanda ya washiriki Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Dkt Francis Michael alikipongeza Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kuanzisha Programu mbalimbali za ujasiriamali zinazowawezesha wanafunzi wa Chuo hicho kujihusisha katika kazi za uzalishaji Mali na kujikwamua kiuchumi.
Akiwa katika banda hilo Dkt. Michael amejionea kazi mbalimbali zinazofanywa na wajasiriamali hao ikiwemo bidhaa za Kilimo pamoja na Ushonaji.
Maonesho ya Taasisi za Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yalifunguliwa rasmi Julai 18, mwaka huu na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa na kufikia tamati yake Julai 23,2022.