Home BUSINESS  RC KIGOMA ARIDHISHWA NA UTENDAJI WA BRELA

 RC KIGOMA ARIDHISHWA NA UTENDAJI WA BRELA

Afisa Usajili wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Bw. Stanslaus Kigosi (kulia), akielezea kuhusu huduma zinazotolewa na BRELA, kwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Thobias Andengenye (kushoto), alipotembelea banda hilo katika Maonesho ya (6), yaliyoandaliwa na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), katika uwanja wa Mwanga, mjini Kigoma. Maonesho hayo ya siku saba yamehitimishwa leo tarehe 27 Mei, 2023.

Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Uwezeshajii Wananchi Kiuchumi (NEEC) Prof. Aurelia Kamuzora, akisaini katika kitabu cha wageni alipotembelea banda la Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), leo tarehe 27 Mei, 2023, kwenye Maonesho ya Sita (6) yaliyoandaliwa na Baraza hilo katika uwanja wa Mwanga, mjini Kigoma.

KIGOMA

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Thobias Andengenye ameipongeza Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), kwa jitihada inazozifanya za kuwezesha wananchi kurasimisha biashara zao na namna inavyotoa huduma katika Maonesho ya sita (6) ya Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC).

Pongezi hizo amezitoa leo tarehe 27 Mei, 2023 alipotembelea banda la BRELA kabla ya kufunga maonesho hayo ambayo yamefanyika katika uwanja wa Mwanga, Mjini Kigoma.

Mhe. Andengenye amesema ameridhishwa na namna BRELA inavyotekeleza majukumu yake, wakati akipatiwa maelezo na Afisa Usajili wa BRELA Bw. Stanslaus Kigosi, juu ya ushiriki wa BRELA katika maonesho hayo.

Akitoa maelezo hayo kwa Mkuu wa mkoa, Bw. Kigosi, ameeleza kuwa katika maonesho hayo mbali na kutoa elimu pia wamekua wakitoa usaidizi kwa wadau mbalimbali kwenye Mfumo wa Usajili kwa njia ya Mtandao, pamoja na kutoa huduma za usajii za papo kwa papo.

“Huduma zote za BRELA zinazotolewa kwa njia ya mtandao, hivyo baadhi ya wananchi wamekuwa wakipata changamoto katika kupata huduma hizo, uwepo wetu hapa ni kuwawezesha kupata huduma hizo zikiwemo Usajili wa Majina ya Biashara, Usajili wa Makampuni na Utoaji wa Leseni za Biashara Kundi “A” papo kwa papo”, amesema Bw. Kigosi.

Aidha Bw. Kigosi amezitaja huduma zingine zinazotolewa na BRELA kuwa ni pamoja na Usajili wa Alama za Biashara na Huduma, Utoaji wa Hataza, Utoaji wa Leseni za Viwanda na huduma baada ya usajili.

Katika maonesho hayo pia maafisa wa BRELA wamepata fursa ya kutembelea mabanda ya washiriki wengine na kuwahamasisha kurasimisha biashara zao.

Maonesho hayo ya siku saba yalianza tarehe 21, Mei, 2023 na yamehitimishwa leo tarehe 27 Mei, 2023.

Maafisa wa Wakala wa Usajili Biashara na Leseni (BRELA), waliovaa fulana zenye nembo ya Wakala, wakikabidhi vyeti vya Usajili wa Majina ya Biashara kwa wadau waliokamilisha taratibu za usajili katika banda la BRELA, kwenye Maonesho yaliyoandaliwa na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC).

Maonesho hayo yamefungwa leo na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma  Mhe. Thobias Andengenye katika uwanja wa Mwanga, mjini Kigoma.

Previous articleWAZIRI UMMY MWALIMU AWAFARIJI WAGONJWA TANGA
Next articleWANAFUNZI WA KIKE WANUFAIKA NA MFUKO WA UDHAMINI WA MWL. NYERERE
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here