Home LOCAL MSIGWA AFUNGUA MAADHIMISHO YA MIAKA 30 YA MISA TANZANIA

MSIGWA AFUNGUA MAADHIMISHO YA MIAKA 30 YA MISA TANZANIA

Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya habari- MAELEZO Gerson Msigwa akizungumza wakati wa Maadhimisho ya Miaka 30 ya Misa Tanzania  yanayofanyika Jijini Dodoma. 

Mwenyekiti wa Misa Tanzania, Salome Kitomari akizungumza wakati wa Maadhimisho ya Miaka 30 ya Misa Tanzania leo Mei 25,2023 Jijini Dodoma.

Mkurugenzi wa Misa Tanzania, Elizabeth Riziki akizungumza wakati wa Maadhimisho ya Miaka 30 ya Misa Tanzania leo Mei 25,2023  Jijini Dodoma.

 Mkurugenzi wa Bodi ya Uongozi ya MISA Kanda, Dk. Tabani Moyo akizungumza wakati wa Maadhimisho ya Miaka 30 ya Misa Tanzania leo Mei 25,2023 Jijini Dodoma.

Mwakilishi wa Internews,Agnes Kayuni akizungumza wakati wa Maadhimisho ya Miaka 30 ya Misa Tanzania leo Jijini Dodoma.

   Sehemu ya washiriki wa Maadhimisho ya Miaka 30 ya Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Jangwa la Sahara Tawi la Tanzania (MISA Tanzania) yakiendelea jijini Dodoma.

Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya habari- MAELEZO Gerson Msigwa ,akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kufungua  Maadhimisho ya Miaka 30 ya Misa Tanzania  yanayofanyika Jijini Dodoma. 

Na: Gideon Gregory, Dodoma.

Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa amefungua Maadhimisho ya Miaka 30 ya Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Jangwa la Sahara Tawi la Tanzania (MISA Tanzania) na akiwasisitiza waandishi wa habari kuzingatia maadili ya uandishi wa habari.

Msigwa amesisitiza hilo leo Mei 25,2023 Jijini Dodoma wakati akimwakilisha Naibu waziri wa Habari, Mawasiliano na Tekonolojia ya Habari, Mhandisi Kundo Mathew wakati wa maadhimisho ya miaka 30 ya MISA.

Amesema serikali inaendelea kuboresha mazingira ya vyombo vya habari huku akisisitiza kuwa tangu Rais Samia Suluhu Hassan aingie madarakani hakuna chombo kilichofungiwa na vilivyokuwa vimefungiwa vimefunguliwa.

Aidha amesema katika kipindi hiki mafunzo au semina kwa waandishi zinahitajika hivyo kuiomba Misa Tanzania na wadau wengine kuwapatia mafunzo mbalimbali waandishi wa habari.

“Katika kipindi hiki tunahitaji sana mafunzo kwa waandishi wa habari. Katika program zetu tuimarishe sana mafunzo kwa waandishi wa habari, Misa Tanzania na wadau wengine tutie mkazo sana kwenye mafunzo kwa waandishi wa habari.Mimi ni miongoni mwa wanufaika wa mafunzo kwa wanahabari ambayo yamekuwa yakitolewa na taasisi ya habari ya MISA-Tanzania”,amesema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Misa Tanzania, Salome Kitomari ,amempongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayofanya ya kuwatumikia Watanzania, lakini zaidi kwa namna amechukua hatua kadhaa zilizowezesha waandishi wa habari kutekeleza majukumu yao kwa kuondoa vikwazo vingi.

Kitomari amesema MISA Tanzania imepita kwenye safari ya miaka 30 yenye milima na mabonde na kutokana na mambo yote hayo ameupongeza uongozi, sekretarieti na wanachama wa MISA Tanzania kwa kushikamana mpaka kufikia hatua hiyo.

“Tuna mengi ya kujivunia ikiwemo kuwa na Ofisi yetu eneo la Kinondoni Mkwajuni, Dar es Salaam na kubaki kwenye DNA ya MISA ya Uhuru wa kujieleza, uhuru wa vyombo vya habari na upatikanaji wa taarifa nchini.Wanachama kutoka taasisi na mwanachama mmoja mmoja,Viongozi waliopita wenye mchango kubwa kwenye tasnia ya habari na Wadau wa Maendeleo kutoka serikali za Canada, Finland, Uingereza, Ujerumani, Marekani na nyinginezo”,amesema.

Sanjari na hayo ameongeza kuwa mafanikio mengine ni pamoja na kutoa mafunzo ya ndani na nje ya nchi kwa waandishi wa habari, Kuwezesha uanzishwaji wa vyombo vingine vya habari zikiwamo Radio za Kijamii na kufanya marekebisho kwenye sheria mbalimbali tangu Sheria ya Magazeti, Sheria ya Huduma za Habari, Sheria ya Haki ya Taarifa na nyinginezo.

“Pamoja na mafanikio mengi miongoni mwa changamoto kubwa zinazoikabili tasnia ya habari nchini ni pamoja na Uchumi wa wanahabari. Pamoja na kwamba ni wajibu wa waandishi wa habari kupasha habari kwa Watanzania lakini wengi wana hali ngumu kimaisha, hawana mikataba, bima za afya na stahiki nyingine za kisheria kama michango kwneye mifuko ya hifadhi ya jamii.Hali hii inaathari kubwa kwenye mchakato wa habari kwa kuwa kunatoa mwanya wa rushwa kwa sababu siku zote tumbo lenye haliwezeshi ubongo kufikiri vyema”,amesema Kitomari.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Misa Tanzania, Elizabeth Riziki amesema Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Jangwa la Sahara,Tawi la Tanzania (MISA Tanzania), inaadhimisha miaka 30 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1993 baada ya kikao cha wanahabari waliokutana Windhoek, Namibia kujadili mambo mbalimbali yaliyokuwa yanaukabili Ukanda wa Nchi za Kusini.

MISA ina matawi tisa katika nchi za Zambia, Msumbiji, Malawi, Lesotho, Botswana, Namibia, Angola, Tanzania na Zimbabwe ambako ndiyo makao makuu ya matawi yote.

“Kwa mwaka huu, MISA Tanzania inaadhimisha miaka 30, MISA inafanya kazi ya kichechemuzi katika uhuru wa Habari, kupata na kutoa taarifa na uhuru wa kujieleza”,amesema Riziki.

“Mwaka huu MISA inafanya maadhimisho hayo kwa kuangalia uchechemuzi wa uhuru wa kujieleza kama msingi wa haki zote na moja ya maeneo makuu ambayo MISA inafanyia kazi; kwa kuangalia namna ulivyokua ukifanyika, unavyofanyika na namna gani tufanye kuboresha kulingana na mabadiliko ya wakati na teknolojia” ameongeza.

Amefafanua kuwa katika mkutano huo wa siku mbili wadau watajadiliana kuhusu kasi ya mabadiliko ya kiteknolojia na namna ambavyo umma unahusishwa kwenye uhuru wa kujieleza na upatikanaji wa taarifa lakini pia watajadili changamoto zilizopo kwenye sekta ya habari na kuweka mkakati wa kuzitatua ikiwamo namna ya kuboresha maisha ya waandishi wa habari.

Pia amesema Majadiliano hayo yana lengo la kuongeza ukaribu na ushirikiano baina ya waandishi wa habari na Jamii, pia kuibua hoja zitakazowaleta pamoja Jamii na waandishi wa habari katika kuwa na mpango kazi wa utekelezaji ili kuhakikisha kila mwanajamii anatumia vizuri nafasi ya uhuru wa kujieleza kupitia vyombo vya habari kwaajili ya maendeleo endelevu.

Ikumbukwe kuwa Misa Tanzania inaadhimisha miaka 30 huku kauli mbiu ikiwa ni “Uhuru wa Kujieleza Msingi wa Haki Zote kwa Maendeleo Endelevu”.

Previous articleRAIS SAMIA, MUSEVENI WAZINDUA MRADI WA KUFUA UMEME WA KIGAGATI, NCHINI UGANDA
Next articlePICHA – MAKAMU WA RAIS AKIONDOKA SHARM EL SHEIKH
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Open chat
GREEN WAVES MEDIA
Ahsante kwa kutembeiea MSIGWA AFUNGUA MAADHIMISHO YA MIAKA 30 YA MISA TANZANIA