Arusha. Tarehe 20 Mei 2023:
Kwenye mkutano wao mkuu wa 28 wa mwaka, wanahisa wa Benki ya CRDB wameidhinisha mapendekezo ya Bodi ya Wakurugenzi ya kulipa gawio la Shilingi 45 kwa kila hisa hivyo kufanya jumla ya gawio kwa mwaka wa fedha 2022 kuwa Shilingi 117.5 bilioni.
Akizungumza kwenye mkutano huo uliofanyika katika katika Kituo cha Kimataifa wa Mikutano Arusha (AICC) huku wengine wakifuatilia ajenda zilizojadiliwa kwa njia ya mtandao, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB, Dkt Ally Laay amesema gawio lililopitishwa ni sawa na ongezeko la 25% likilinganishwa na gawio la Shilingi 36 kwa hisa lililolipwa mwaka jana hali inayodhihirisha kuendelea kuimarika kwa pato kwa hisa ambalo mwaka 2022 limefika TZS 134.5.
“Kwa mara nyingine tena, tunafurahi kupata matokeo mazuri kwa mwaka 2022 yaliyochangia kuongeza thamani kwa wanahisa wetu. Faida tuliyoipata mwaka 2022 ni uthibitisho wa utekelezaji makini wa mpango mkakati wetu wa miaka mitano wa 2018 – 2022. Benki ilipata faida ya baada ya kodi ya Shilingi 351.4 bilioni sawa na ongezeko la 31% ikilinganishwa na Shilingi 268.2 bilioni za mwaka 2021,” amesema Dkt Laay.
Vilevile, Dkt. Laay amesema kampuni tanzu ya Burundi nayo inazidi kuimarika hivyo kuwa na mchango mkubwa zaidi kwenye faida ya kampuni mama. Kwa mwaka 2022, amesema Benki ya CRDB Burundi imepata faida kubwa zaidi tangu lilipoanzishwa mwaka 2012. Kampuni hiyo tanzu ilipata faida ya Shilingi 23 bilioni mwaka 2022 ambayo ni sawa na ongezeko la 79.7% kutoka Shilingi 12.8 bilioni iliyopatikana mwaka 2021. Kwa faida hiyo, kampuni tanzu hiyo ilichangia 7.0% kwenye faida ya kampuni nzima.
“Nina furaha kuwataarifu kwamba hivi karibuni tumepata leseni ya kuanza kutoa huduma za fedha kutoka Benki Kuu ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (BCC). Vilevile, Benki yetu imeanzisha kampuni tanzu mbili mwaka huu ambazo ni CRDB Bank Foundation na CRDB Insurance Company ikiwa ni benki ya kwanza kuanzisha kampuni tanzu kamili a bima,” amesema Dk Laay.
Akizungumzia utendaji wa Benki, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema katika mwaka wa fedha 2022, waliendeleza juhudi za kukuza mapato na wakafanikiwa kwa kiasi kizuri kwani mapato ya uendeshaji yaliongezeka kwa 28% na kufika Shilingi 745.8 bilioni yakichangiwa na kuongezeka kwa mikopo iliyotolewa. Kwa mwaka 2022, uwiano wa mikopo chechefu ulishuka mpaka 2.8% hivyo kuwa ndani ya ukomo uliowekwa kikanuni wa kutozidi 5%.
Mizania ya Benki pia, amesema ilikua kwa 32% kutoka Shilingi 8.8 trilioni mwaka 2021 mpaka Shilingi 11.6 trilioni hivyo kuwa taasisiya kwanza ya fedha nchini kuvuka Shilingi 10 trilioni. Ongezeko hilo, amesema limechangiwa na kuimarika kwa amana za wateja zilizoongezeka kwa 26.4% na kufika TZS 8.2 trilioni kutoka TZS 6.5 trilioni za mwaka 2021.
“Juhudi zetu za kuimarisha huduma zetu zilituletea mafanikio hasa katika kubana matumizi kwani uwiano wa gharama na mapato uliimarika kutoka 66.7% mwaka 2018 mpaka 49.4% mwaka 2022,” amesema Nsekela.
Nsekela amesema ufanisi uliopatikana umewezesha kuwekeza zaidi kuimarisha huduma kwa kuwekeza kwenye majukwaa ya kidijitali ambayo yanasaidia kukidhi mahitaji ya wateja kwa kuwapa huduma wazitakazo mahali walipo na kuzitumia kwa namna waitakayo. “Leo hii zaidi ya 95% ya miamala yote ya benki inafanyika kidijiti hasa kupitia SimBanking, huduma za benki kwa intaneti, na kwa zaidi ya mawakala 28,000 wa Benki ya CRDB,” ameongeza.
Katika miaka mitano iliyopita, amesema Benki ilianzisha ubia wa kimkakati ambao umechangia kwenye mafanikio yake kwa mwaka 2022. Katika kipindi hicho, ubia huo umeiwezesha Benki ya CRDB pamoja na kampuni tanzu zake kukuza mtaji, kuwa na teknolojia ya kisasa na kuboresha huduma hivyo kukidhi matarajio ya wateja.
Kuhusu mikakati ya baadae, Nsekela amesema Bodi ya Wakurugenzi imeidhinisha mpango mkakati wa miaka mitano kuanzia mwaka 2023 – 2027 unaosisitiza kujenga uchumi shirikishi, kuongeza thamani endelevu kwa wanahisa, na kuingia katika ubia wa kimkakati ili kuikuza Benki na kuongeza ushawishi wake sokoni.
Mpango mkakati huo, amesema umetanguliza mbele maslahi ya wateja jambo linalomaanisha Benki sasa inawekeza katika kuyatambua mahitaji ya wateja na kuyafanyia kazi ili kukidhi matarajio yao.
Nsekela amewashukuru wanahisa wa Benki hiyo kwa ushirikiano ambao wameendelea kuipatia menejimenti na wafanyakazi wa benki hiyo, na kuwawathibitishia kwamba Benki itaendelea kufanya vizuri ili kuwapa thamani ya uwekezaji walioufanya na wanaoendelea kuufanya.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Dkt Ally Laay amesema mwaka 2022 walifanya mabadiliko kadhaa ya menejimenti yanayoendana Sera mpya ya Rasilimali Watu. Katika mabadiliko hayo, Bwana Boma Raballa aliyekuwa Mkurugenzi wa Wateja Wadogo alipandishwa cheo na kuwa Afisa Mkuu wa Biashara akichukua nafasi ya Dkt Joseph Ochieng Witts aliyestaafu.
Kutokana na kupandishwa cheo kwa Bwana Raballa, amesema Bodi iliamteua Bwana Bonaventure Paul kukaimu ukurugenzi wa wateja wadogo. Vilevile, Bwana Godfrey Rutasingwa aliyekuwa anakaimu ukurugenzi wa Rasilimali Watu, alithibitishwa katika nafasi hiyo.
Kwa upande mwingine, wanahisa walipitisha kampuni ya Ernst & Young kuwa mkaguzi wa nje wa hesabu za fedha kwa mwaka 2023. Vilevile, wanahisa hao waliwachagua kwa mara nyingine tena Profesa Neema Morina Miranda Naiman Mpogolo kuwa Wajumbe Huru wa Bodi ya Wakurugenzi.
Akizungumzia gawio lililoidhinishwa, Mkurugenzi Mtendaji mstaafu wa Benki ya CRDB ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Vunjo, Dkt Charles Kimei amesema wanahisa wamefurahia ongezeko la gawio lililopendekezwa. Dkt. Kimei aliongezea kuwa kitendo cha Benki ya CRDB kutoa gawio kiila mwaka kimekuwa kikiwavutia wawekezaji wengi ndani na nje ya nchi kuwekeza ndani katika hisa za benki hiyo.