Home BUSINESS WACHIMBAJI WA DHAHABU MGODI WA LUKALASI WAPELEKEWA HUDUMA YA UCHUNGUZI WA KIFUA...

WACHIMBAJI WA DHAHABU MGODI WA LUKALASI WAPELEKEWA HUDUMA YA UCHUNGUZI WA KIFUA KIKUU

 
Mratibu wa kifua kikuu na ukoma wa Halmashauri ya wilaya Mbinga Dkt Bryson Mapunda akitoa elimu ya kifua kikuu kwa wachimbaji wadogo wa dhahabu katika eneo la Lukalasi wilaya Mbinga kabla ya kuanza kwa zoezi la uchunguzi wa vimelea vya ugonjwa huo katika kampeni maalum ya uelimishaji na upimaji inayofanywa na Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo shirika la Management and Development for Heath(MDH).

Baadhi ya wachimbaji wadogo wa dhahabu katika mgodi wa Lukalasi kata ya Kigonsera Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma unaomilikiwa na mwekezaji mzawa Jonson Nchimbi wakisubiri huduma ya uchunguzi wa vimelea vya kifua kikuu wakati wa kampeni ya uelimishaji na uchunguzi wa ugonjwa huo iliyofanywa na Madaktari wa Halmashauri ya wilaya Mbinga na wataalam wa shirika la Management and Development for Heath(MDH).
Wananchi wanaoishi na kufanya shughuli za uchimbaji madini ya dhahabu katika mgodi wa Lukalasi kata ya Kigonsera wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma wakisubiri kupata huduma ya uchunguzi wa ugonjwa wa kifua kikuu kutoka kwa Madaktari wa Halmashauri ya wilaya Mbinga na wataalam kutoka shirika la MDH.

Na: Muhidin Amri, Mbinga

WACHIMBAJI wadogo wa dhahabu wanaofanya shughuli zao  katika kijiji cha Lukalasi kata ya Kigonsera wilayani Mbinga,wameiomba Serikali  kuwasogezea  Huduma za Afya kwa kujenga zahanati au kituo cha Afya ili waweze kupata  huduma za matibabu ikiwemo za kifua kikuu na chanjo ya Covid-19.

Wametoa maombi  hayo jana, wakati wa  zoezi la kampeni ya uibuaji na upimaji wa vimelea vya ugonjwa wa kifua kikuu(TB) kwenye machimbo inayofanywa na Hospitali ya Halmashauri ya wilaya Mbinga  na wataalam wa shirika la Management and Development for Heath(MDH).

Akizungumza kwa niaba ya wachimbaji hao Elimwaria Muro alisema, katika eneo hilo kuna watu zaidi ya  elfu mbili wanaofanya kazi ya kutafuta na kuchimba  dhahabu lakini  hakuna huduma za afya.

Hivyo alisema, wakati umefika kwa Serikali kupitia wizara ya afya kuwajengea zahanati au kituo cha afya ili jamii inayoishi eneo hilo waweze kupata huduma za matibabu jirani na  makazi yao.

Kwa mujibu wa Muro,iwapo Serikali itasogeza huduma za afya katika eneo hilo jamii itakuwa na afya njema  na kuwawezesha kushiriki kazi mbalimbali za maendeleo na  kutoa mchango mkubwa kujenga uchumi wa nchi yao.

Aidha Muro ambaye ni Mhandisi wa mgodi wa dhahabu wa Lukalasi unaomilikiwa na mzawa Jonson Nchimbi, ameipongeza Serikali  kupitia wizara ya afya kupeleka huduma ya uchunguzi  wa ugonjwa wa kifua kikuu kwa kutumia cliniki inayotembea(Mobile Clinic) kwa wananchi waishio maeneo ya machimbo ya  madini.

Nchimbi alisema, kwa sasa wanalazimika kutembea umbali mrefu hadi kijiji cha Kigonsera au Mbinga mjini  kufuata matibabu,jambo ambalo ni kero  kubwa na linawapotezea muda mwingi wa kufanya kazi za maendeleo.

Naye Dkt Bingwa wa magonjwa ya ndani ya Binadamu Dkt Dennis Ngatenelela alisema,serikali imelazimika kutumia cliniki inayotembea kuwafikia wananchi wanaoishi maeneo ya pembezoni ili waweze kupata huduma mbalimbali za afya.

Alisema, mpango wa Serikali kupitia wizara ya afya ni kuhakikisha kila mtu anapata huduma  pale alipo na hakuna mwananchi atakayepoteza maisha kwa kukosa matibabu,ndiyo maana wamelazimika kupeleka huduma za uchunguzi hadi katika maeneo  hayo.

Akizungumzia ugonjwa wa kifua kikuu Dkt Dennis alisema, tafiti za kitaalam zinaonesha kuwa kuna uhusiano wa karibu kati ya shughuli za uchimbaji wa madini na ugonjwa wa kifua kikuu kutokana na vumbi linalotoka wakati wa kutafuta na kuchimba madini kuingia  ndani ya mwili wa Binadamu.

Alisema,wadudu wa kifua kikuu mara nyingi wanakaa katika miili ya binadamu na ugonjwa huo unatibika kwa mtu aliyeambukizwa kupata matibabu yanatolewa bure katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya.

Kwa upande wake mratibu wa kifua kikuu na ukoma wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga Dkt Bryson Mapunda alisema, matibabu ya kifua kikuu ni ya miezi sita na mgonjwa anatakiwa kunywa dawa kila siku bila kuacha.

Alisema, ni muhimu kumaliza dozi au matibabu kama ilivyoelekezwa na muhudumu wa afya na kuonya kuwa, kuacha kunywa dawa kikamilifu kuna weza kusababisha vimelea kuwa sugu na hivyo kuambukiza watu wengine.

Dkt Mapunda alisema, kifua kikuu sio ugonjwa wa kulogwa wala kurithi bali ni ugonjwa unaoambukizwa na vimelea aina ya bakteria visivyoonekana kwa macho bali kwa kutumia hadubini.

Amewashauri, watu wenye dalili za ugonjwa huo  kuwahi kwenye kituo cha kutolea huduma za afya kwa ajili ya uchunguzi na kifua kikuu kinatibika na kupona kabisa hata kama ana mgonjwa maambukizi ya virusi vya ukimwi.

Alisema, mtu anapaswa kupata matibabu  mapema ili kuzuia maambukizi kwa wengine na mgonjwa ambaye ameanza tiba sio rahisi kuambukiza mtu mwingine,hivyo hakuna sababu ya kumtenga.
MWISHO.

Previous articleRAIS MUSEVEN AWASILI NCHINI KUANZA ZIARA YA KISERIKALI YA SIKU TATU
Next articleTMDA YATOA TATHIMINI YA UTEKELEZAJI WA MWAKA MMOJA WA MRADI WA ASCEND
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here