Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Balozi Wilbert Ibuge akiongea jana na wananchi na viongozi wa wilaya ya Mbinga baada ya kufungua zahanati ya kijiji cha Ruanda wilaya ya Mbinga,katikati Mkuu wa wilaya hiyo Aziza Mangosongo na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Juma Haji.
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Balozi Wilbert Ibuge katikati aliyevaa kofia na viongozi mbalimbali wa wilaya ya Mbinga wakikata utepe kuashiria ufunguzi rasmi wa Zahanati ya kijiji cha Ruanda Halmashauri ya wilaya ya Mbinga,wa kwanza kulia Mbunge wa jimbo la Mbinga Mjini Jonas Mbunda,wa pili kulia Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya Mbinga Juma Haji na Mkuu wa wilaya hiyo Aziza Mangosongo wa pili kushoto.
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Balozi Wilbert Ibuge kulia,akicheza ngoma ya kihoda na baadhi ya wakazi wa kijiji cha Ruanda kata ya Ruanda wilaya ya Mbinga kabla ya kufungua zahanati iliyojengwa kwa nguvu za wananchi kwa kushirikana na Serikali.
Baadhi ya wanafunzi wa shule ya msingi Ruanda Halmashauri ya wilaya Mbinga mkoani Ruvuma wakiimba wimbo maalum wa kuipongeza Serikali na wazazi kwa kufanikisha ujenzi wa zahanati katika kijiji hicho ambayo imesaidia kusogeza na kuboresha huduma za afya kwa wananchi.
Wakazi wa kijiji cha Ruanda kata ya Ruanda Halmashauri ya wilaya Mbinga mkoani Ruvuma wakicheza ngoma ya Kioda wakati wa ufunguzi wa zahanati iliyojengwa kwa nguvu zawananchi na Serikali kwa gharama ya zaidi ya Sh.milioni 91
Picha zote na Muhidin Amri,
Na Muhidin Amri,Mbinga
MKUU wa mkoa wa Ruvuma Balozi Wilbert Ibuge, amefungua zahanati ya kijiji cha Ruanda kata ya Ruanda katika Halmashauri ya wilaya Mbinga iliyojengwa kutokana na michango ya wananchi,Serikali na wadau wengine wa maendeleo.
Balozi Ibuge, amewapongeza wananchi hao kwa kuamua kutatua kero zao wenyewe bila kusubiri msaada wa serikali kwa kuchangia Sh. milioni 16 jambo linalopaswa kuigwa na wananchi wa maeneo mengine.
Mkuu wa mkoa alisema, zahanati hiyo ni mkombozi mkubwa kwa wananchi na kuwataka kuhakikisha wanaitunza na kulinda mindombinu ili ilete manufaa na kusisitiza kuwa,Serikali itaendelea kushirikiana na wananchi katika shughuli zote za maendeleo.
Aidha Ibuge, amefurahishwa na kazi nzuri za maendeleo zinazofanywa na wananchi wa wilaya ya Mbinga na kuhaidi kuwa,serikali ya mkoa itaendelea kushirikiana na wananchi walioonyesha jitihada za kumaliza changamoto zao.
Amewataka,viongozi kuanzia ngazi ya vijiji,kata,na Wabunge kujitolea na kushiriki kazi mbalimbali za maendeleo zinazolenga kumaliza changamoto na kero zinazowakabili wananchi.
Diwani wa kata ya Ruanda Deogras Mwingira alisema,wananchi wa kijiji hicho waliokuwa wanakabiliwa na kero ya upatikanaji wa huduma za afya kwa kipindi kirefu,sasa wameondokana na changamoto hiyo baada ya kukamilika kwa ujenzi wa zahanati hiyo iliyoanza kujengwa tangu mwaka 2013.
Alisema,zahanati hiyo itawapunguzia wananchi wa kijiji cha Ruanda na vijiji vya jirani kero na adha waliyokuwa wanaipata kwa muda mrefu ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma za matibabu katika mengine.
Ameishukuru serikali na wadau waliofanikisha ujenzi huo,kuunga mkono juhudi za wananchi katika kusaidia na kuboresha sekta ya afya kwa wananchi ambao walikaa kwa muda mrefu kusubiri huduma za matibabu.
Afisa Mtendaji wa kijiji cha Ruanda Idrisa Machumu alisema,ujenzi wa zahanati hiyo umefanyika kwa awamu tofauti na mpaka kukamilika jumla ya Sh.milioni 91,875,000.00 zimetumika.
Machumu alisema,Halmashauri ya wilaya kupitia mapato yake ya ndani imetoa Sh milioni 25,Serikali kuu imetoa Sh.milioni 50 na wananchi wamechangia Sh.milioni 16,875,000.00 ambapo zaidi ya wakazi 5,700 watanufaika.
Alisema, uwepo wa zahanati hiyo utapunguza vifo vya akina mama wajawazito na watoto walio chini ya umri wa miaka mitano na kusaidia upatikanaji dawa,vifaa tiba, na vifaa saidizi kuimarisha na kusogeza huduma za afya kwa wananchi wa kijiji na kata ya Ruanda.
MWISHO.