Home LOCAL ITUMIENI KAMPENI YA HUDUMA YA MSAADA WA KISHERIA YA MAMA SAMIA –...

ITUMIENI KAMPENI YA HUDUMA YA MSAADA WA KISHERIA YA MAMA SAMIA – MAJALIWA

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka watanzania kuitumia kampeni ya Huduma ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia kutoa taarifa kuhusu uwepo wa watu, au vikundi vya watu ambao ama wanajihusisha na ukatili wa kijinsia hususan kwa watoto.

Ametoa wito huo leo Alhamisi (Aprili 27, 2023) alipozindua kampeni hiyo ambayo itatekelezwa kwa miaka mitatu kuanzia Machi, 2023 hadi Desemba 2025.

Amesema kuwa kampeni hiyo itasaidia kuongeza uelewa wa sheria na upatikanaji haki, mifumo ya utoaji haki, masuala ya kisheria na haki za binadamu kwa kushirikiana na taasisi za serikali, asasi za kiraia na wadau wa maendeleo katika utoaji huduma kwa wananchi.

“Kampeni hii pia itasaidia kuboresha upatikanaji wa haki kwa watu wasiojiweza, hususani wanawake, watoto na makundi mengine yaliyo katika mazingira magumu. Vilevile, itachangia kuimarisha amani na utulivu, kuongeza kipato cha mmoja mmoja na kuleta utengamano wa kitaifa”.Amesema

Ameongeza kuwa, faida nyingine ya kampeni hiyo ni kusaidia kuimarisha mfumo wa utoaji wa huduma ya msaada wa kisheria katika ngazi zote yaani kuanzia Serikali kuu hadi Serikali za Mitaa. “Ushiriki wa wadau wanaojihusisha na huduma ya msaada wa kisheria utaongezeka kwa asilimia 80 katika ngazi za Serikali Kuu hadi Serikali za Mitaa”

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Katiba na Sheria iweke mfumo mzuri wa kushughulikia changamoto za kisheria zitakazoibuliwa wakati wa Kampeni katika utimilifu wake.“Tusiache wananchi wakiwa bado hawajapata majibu ya changamoto zao. Hii itasaidia kujenga taswira nzuri kwa Serikali wala kwa mamlaka ambayo imeridhia kuwepo kwa Kampeni hii”

Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa ameitaka Wizara hiyo itekeleze majukumu yake kwa ufanisi na weledi mkubwa ili Watanzania wote waweze kuifikia haki na kuipata haki kwa wakati.

“Kwa wale ambao hawawezi kumudu gharama za mawakili wa kujitegemea hakikisheni wanapata huduma za kisheria bila ya upendeleo wowote na kwa viwango stahiki”.

Previous articleRAIS SAMIA AKUTANA NA KUZUNGUMZA NA RAIS WA RWANDA PAUL KAGAME, IKULU JIJINI DAR ES SALAAM
Next articleDAWASA YAFUNGUA DAWATI LA HUDUMA KWA WATEJA
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here