Punda wakiwa kwenye malisho. |
Na: Boniphace Jilili,Singida.
JAMII mkoani Singida zinazojishughulisha na ufugaji, zimeipongeza Serikali kwa hatua ya kufunga Kiwanda cha kuchinja Mnyama Punda mkoani Shinyanga kwani kilitishia kuwamaliza kabisa wanyama hao ambao takwimu zinaonyesha kuwa wachache kuliko wanyama wengine.
Hivi karibu Serikali kupitia Wizara yenye dhamana ya mifugo ilikifunga kiwanda hicho cha kuchinja mnyamakazi punda kilichopo mkoani Shinyanga kwa lengo la kuwanusuru wanyama hao wasiendelee kuisha.
Awali Shirika lisilo la kiserikali la Inades Formation Tanzania (IFTz) lenye Makao makuu yake Dodoma lilianza jitihada za kuhakikisha jamii inamthamini mnyama huyo kupitia mradi wake wa kumtetea mnyama Punda kwa kutoa elimu ya umuhimu wa Mnyama huyo kutokana na mnyama huyo kutothaminiwa na kutopewa kipaumbele katika mipango ya maendeleo ngazi mbalimbali za jamii na Serikali.
Jamii nyingi hazikuwa zinamthamini Punda licha ya kuwa msaada mkubwa kwao katika shughuli mbalimbali za maendeleo hasa katika masuala ya usafiri ndio maana ilipelekea hata kuuzwa kwa bei ndogo mno na hamasa ndogo ya kumfuga.
Mratibu wa mradi wa ustawi wa Punda Fortunata Tarimo kutoka shirika hilo alisema kwa mda wa Miaka Miwili sasa wamekua wakitoa elimu kwa Jamii juu ya ustawi wa Mnyama Punda ambapo takribani Vijiji Vitano katika Halmashauri ya Singida mkoani Singida wamepata elimu hiyo na kuona umuhimu wa mnyama huyo.
“Jamii nyingi sasa zinahakikisha zinampatia malisho,zinampatia matibabu kama wanyama wengine tofauti na kipindi cha nyuma haya yote yamefanyika baada ya jamii kutambua umuhimu wa Mnyama Punda katika shughuli mbalimbali za maendeleo.” alisema mratibu.
Hata hivyo mratibu huyo alisema Shirika limefurahishwa na tamko la Serikali la kuyafungia Machinjio ya mnyama Punda huko mkoani Shinyanga na wao kama wadau wataendelea kuiunga mkono Serikali kuhakikisha mnyama huyo analindwa ili kuendelea kuwa na tija katika jamii.
Akielezea hatua ya Serikali kuyafunga Machinjio hayo kaimu Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Endeshi Emanuel Michael alisema zilikuwa zinaripotiwa kesi nyingi ofisini kwake zinazomhusisha mnyamakazi punda ambapo watu walishitakiana kuhusu kupotea punda waliokuwa wakipelekwa Shinyanga kuchinjwa.
Alisema anashukuru Serikali kwa hatua hiyo kwani inaenda kuondoa kesi hizo na kupelekea ustawi wa mnyama huyo kuongezeka kwa maslahi ya jamii kutokana na kutumika kama, Usafiri unaopita kila mahali bila kukwama.
“Siku zote Punda huwa wachache unakuta mtu kafuga ngo’mbe 100 punda watatu au watano,sasa walikuwa wanaisha kabisa.” alisema Michael.
Naye mhudumu wa afya ya ustawi wa mnyamakazi punda kutoka Kijiji cha Endeshi Joel Richard alikiri kuwa punda alikuwa hahudumiwi vizuri lakini baada ya jamii kuwezeshwa elimu ya umuhimu wa mnyama huyo kupitia Shirika la Inades sasa anahudumiwa vizuri na kutunzwa na tija imeongezeka.
Alisema kupitia shirika hilo amekuwa akiitwa kila mahali kwenda kutoa huduma ya kitabibu kwa mnyama huyo anapopata tatizo la kiafya na ndio inathihirisha kuwa jamii imetambua umuhimu wa mnyama huyo.
Kwa upande wake Anastasia Joseph mkazi wa Kijiji cha Ghata kilichopo Halmashauri ya Singida alisema punda amekua msaada mkubwa kwa akina mama kwa kubeba maji,kuni na shughuli zingine hivyo akaishukuru Serikali pamoja na Inades kwa juhudi za kuhakikisha punda anaendelea kuwepo.