Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango ameiagiza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuhakikisha wanaweka utaratibu maalumu wa maafisa mifugo kuanzia ngazi ya kata kuwatambua wafugaji na idadi ya mifugo yao ili kuboresha huduma za ugani na kuongeza tija ya mifugo katika Taifa.
Makamu wa Rais amesema hayo leo tarehe 11 Aprili 2023 alipotembelea shamba la mifugo la mabuki na Kituo Atamizi cha Mabuki kinachotumika kunenepesha ng’ombe wa nyama pamoja na mpango wa mafunzo ya ujasiriamali kupitia sekta ya mifugo kilichopo Misungwi mkoani Mwanza.
Amesema ni wakati sasa wa kuhakikisha mifugo mingi iliopo nchini inapata thamani kwa kukuzwa katika ubora unaohitajika na hivyo kuweza kupata masoko nje ya nchi.
Ameongeza kwamba sekta ya mifugo ni fursa kwa vijana na taifa kwa ujumla hivyo ameagiza kudhibitiwa uvamizi katika eneo la Shamba la Mifugo la Mabuki ambalo ni la kimkakati linalotumika kubadilisha sekta ya mifugo nchini.
Akizungumza katika kituo atamizi cha mabuki ambacho kinatumika kunenepesha ng’ombe wa nyama pamoja na mpango wa mafunzo ya ujasiriamali kupitia sekta ya mifugo, Makamu wa Rais ametoa rai kwa wanafunzi na walimu katika vyuo vya kilimo na mifugo hapa nchini kuongeza jitihada katika kutekeleza kwa vitendo kile wanachojifunza na kufundisha.
Amesema wahitimu na wakufunzi katika sekta ya mifugo wanapaswa kuwa mstari wa mbele ili kuongeza tija ya haraka katika sekta hiyo.
Ameongeza kwamba kituo hicho atamizi ni chachu ya mabadiliko katika sekta ya mifugo kitakachosaidia kuondokana na changamoto ya mauzo hafifu ya nyama nje ya nchi licha ya uwepo wa wingi wa mifugo hapa nchini.
Katika kituo hicho ng’ombe waliokonda hununuliwa katika minada na kisha kunenepeshwa kwa kipindi cha miezi mitatu na kuuzwa kwa bei ya faida zaidi.
Mpango huo wa mafunzo ni wa mwaka mmoja ambapo kila kijana atapata fursa ya kunenepesha mifugo katika mizunguko minne ya ng’ombe 10 katika kila mzunguko na faida itakayopatikana itatumika kama mtaji kwaajili ya kijana mnufaika kwena kuanzisha miradi kama hiyo mara baada ya mafunzo.
Kwa upande wake Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega amesema wizara hiyo imejiwekea malengo ya kuhakikisha inatekeleza mazoezi ya kitaifa kama vile chanjo kwa mifugo pamoja na kuwatumia vema maafisa mifugo na vitendea kazi walivyopewa ili viweze kutumika kwa malengo yaliokusudiwa.
Waziri Ulega ameongeza kwamba Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeanza kutekeleza afua ambazo zinatoa mwelekeo mpya wa sekta ya mifugo ili kukabiliana na changamoto zilizopo ikiwemo kuimarisha shughuli za utafiti na mafunzo,kuimarisha biashara na masoko ya mifugo na mazao yake pamoja na upatikanaji wa malisho na maji kwaajili ya mifugo.
Jumla ya ng’ombe 500 aina ya mitamba wamenunuliwa na Serikali ya Awamu ya Sita na kukabidhiwa katika shamba hilo. Shamba la kuzalisha mifugo la Mabuki linamilikiwa na Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi lilianzishwa mwaka 1967 kwa dhumuni la kuzalisha na kusambaza mitamba bora ya ng’ombe wa maziwa kwa wafugaji kwa bei nafuu ili kuwaongezea kipato na kupunguza umasikini kwa jamii.