Na: WAF – Bungeni Dodoma
Naibu Waziri wa Afya Mhe. Godwin Mollel amesema kuwa Serikali imenunua magari 727 ya kubebea wagonjwa na magari 146 kwa shughuli za kiutawala, huku akibainisha tayari magari 20 yamepokelewa na magari 117 yapo njiani kutoka kwa mtengenezaji.
Amesema, katika kuboresha huduma za afya nchini, Serikali ya Rais Samia imehakikisha hakuna Wilaya itayokosa gari la kubebea wagonjwa kutokana na ununuzi wa magari hayo yatayosaidia kuondoa kero za wananchi wenye uhitaji hasa uhitaji wa huduma za rufaa kutoka kituo kimoja kwenda kingine.
Dkt. Mollel amesema hayo leo Aprili 5, 2023 wakati akijibu swali la Mbunge wa viti maalumu Ruvuma Mhe. Mariam Madalu Nyoka katika Mkutano wa 11 kikao cha pili Jijini Dodoma.
Ameendelea kusema kuwa, magari yote yanatarajiwa kuwasili nchini na kukabidhiwa kwenye vituo vya kutolea huduma kabla ya mwezi Juni 2023, huku akisisitiza Wizara ya afya itashirikiana na OR – TAMISEMI ili kufikia maeneo yote yenye uhitaji zaidi kulingana na mazingira.
Aidha, Dkt. Mollel amesema hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa hospitali zitazonufaika na magari hayo kutokana na uhitaji mkubwa katika Mkoa huo kwenye vituo vya kutolea huduma kuanzia ngazi ya zahanati mpaka Mkoa.
Mwisho