Na: stella Kessy, DSM.
UONGOZI wa KMC Umemtangaza kocha Thierry Hitimana (42) raia wa Rwanda kuwa Kocha Mkuu wa kikosi hicho, huku Jonh Simkoko na Habibu Kondo wakifungashiwa virago.
Hitimani amekabidhiwa majukumu ya kukinoa kikosi hicho kwa mkataba wa mwaka mmoja.
Akizungumza na wanahabari Mwenyekiti wa Bodi ya KMC, Meya wa Manispaa wa Kinondoni, Songolo Mnyonge amesema kuwa lengo la kubadilisha benchi la ufundi ni kurudisha kikosi katika hali ya ushindani.
“Tumempa mkataba wa mwaka mmoja kwa ajili ya kurudisha kikosi katika ushindani pia tuna matumaini kuwa atarudisha kikosi katika ushindani ambayo kama ilivyokuwa kwa misimu miwili nyuma, “ amesema.
“Kikosi chetu kipo imara na wachezaji wazuri wenye uwezo hivyo tunaimani kocha huyu atarudisha kikosi kwenye ushindani ambao kilikuwa awali,”amesema.
Kwa upande wake, kocha Hitimana amesema kuwa anaimani na kikosi ambacho anaenda kukinoa.
Amesema kuwa amekubali kufanya kazi tutokana na vipengele vilivyopo katika mkataba pia atajitahidi kufanya kazi kulingana na uzoefu wake na kushirikiana na viongozi pamoja na wachezaji wake.
“Naomba nieleweke kuwa nitafanya kazi kwa kishirikiana na wachezaji pamoja na viongozi ili kukirudisha kikosi katika hali ya ushindani kwani tukishirikiana kwa pamoja tunaweza kufanya mambo makubwa japo ni mapema kusema hivyo,” amesema.
Ikumbukwe kuwa Hitimana alivunja mkataba wake na Simba ambapo alikuwa kocha msaidizi.