Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) amekutana na kuzungumza na Balozi wa Marekani nchini, Mhe. Michael Battle katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.
Pamoja na mambo mengine, viongozi hao wamejadili kuhusu maandalizi ya ziara ya Makamu wa Rais wa Marekani nchini, Mhe. Kamala Harris, masuala ya ushirikiano kati ya Tanzania na Marekani na jinsi ya kufanya kazi kwa pamoja katika kuendeleza uhusiano wa kidiplomasia uliopo baina ya mataifa hayo mawili.
Dkt. Tax ameishukuru Serikali ya Marekani kwa kushirikiano na Serikali ya Tanzania wakati wote tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya mataifa hayo na umekuwa na maslahi mapana kwa wananchi wa pande zote mbili.
Naye Balozi wa Marekani Nchini, Mhe. Battle ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kudumisha uhusiano wake na Serikali ya Marekani.
Katika tukio jingine, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.) amekutana kwa mazungumzo na Balozi wa Urusi nchini Mhe. Mhe. Andrey Avetisyan katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.
Mhe. Balozi Mbarouk ameipongeza Urusi kwa fursa za masomo zinazotolewa na nchi hiyo kwa watanzania na kuomba fursa zaidi za ushirikiano katika sekta za kilimo, madini, afya na uhandisi.
Naye Balozi wa Urusi Mhe. Andrey Avetisyan amesema Serikali ya Urusi inategemea kuongeza idadi ya ufadhili wa nafasi za masomo kutoka idadi ya nafasi 90 hadi 120 ili kutoa nafadi zaidi kwa watanzania kunufaika na fursa za elimu zinazopatikana nchini Urusi.
Urusi imekuwa ikishirikiana na Tanzania katika nyanja mbalimbali hususan sekta za elimu, afya, utalii na utamaduni, mafuta na gesi, ulinzi na usalama, madini, kilimo na uhandisi.