Na: Wizara ya Afya – Dar es salaam.
Serikali imepokea msaada wa Dawa zenye thamani ya Mil. 341 kwa ajili ya kampeni ya minyoo pamoja na kuongeza virutubisho kwenye mwili kutoka katika shirika la World Vision Tanzania.
Dawa hizo zimepokelewa na mkurugenzi wa huduma za dawa na mfamasia mkuu wa Serikali Daudi Msasi akiwa amemuwakilisha katibu mkuu Prof. Abel Makubi.
“Tumepokea Dawa hizi kwa sababu ya mahusiano mazuri ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuimarisha mashirika mbalimbali nchini”. Amesema Msasi.
Bw. Msasi amesema Dawa hizi zimekuwa zikitolewa mara mbili kwa mwaka (mwezi June na Desemba) kwa lengo la kupunguza na kukabiliana na kiasi cha minyoo kwenye miili ya watoto ili wasiwe na upungufu wa Damu.
Aidha, Bw. Msasi amewashauri wananchi kuwapeleka watoto kupata Dawa hizo ifikapo muda wa kugawa mwezi wa sita mwaka huu ili kukinga miili yao na minyoo pamoja magonjwa mengine.
Kwa upande wake Mkurugenzi mwandamizi wa shirika la World Vision Tanzania Dkt. Joseph Mitinje amesema shirika hilo linafanya kazi na Serikali kupitia wizara zake ili kuboresha huduma mbalimbali kwa watanzania bila kujali matabaka.
“Mchango huu umepatikana kwa ushirikiano wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, World Vision ya Serikali ya Marekani pamoja na World Vision ya Serikali ya Canada katika kuhakikisha dawa hizo zinapatikana”.Amesema Dkt. Mitinje.
Hata hivyo Dkt. Mitinje amemshukuru Rais Samia kwa kazi nzuri na kubwa anayoifanya kuhakikisha kuwa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali yanapata nafasi katika kushiriki shughuli za maendeleo.
Nae Mkurugenzi mkuu Bohari ya Dawa Brig. Jen. Dkt. Gabriel Sauli Mhidize ameihakikishia Serikali kuwa Dawa hizo zitalindwa na kusambazwa mapema kwenye maeneo yenye uhitaji nchini.
“Niwashukuru World Vision kutoa msaada wa dawa hizi zitakazo kwenda kuwasaidia watoto wetu na nitazilinda hadi pale zitakapofikia hatua ya kuzigawa“. Amesema Dkt. Mhidize.
Mwisho