Home BUSINESS BIDHAA MPYA YA STAMICO *COAL BRIQUETTE* YATIA FORA ZANZIBAR

BIDHAA MPYA YA STAMICO *COAL BRIQUETTE* YATIA FORA ZANZIBAR

Na: Bibiana Ndumbalo.

Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limebuni mkaa mbadala wa makaa ya mawe ujulikanao kwa jina la Rafiki Briquette unaotarajiwa kuuzwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo Zanzibar.

Mkaa huo umewavutia wananchi wengi waliotembelea banda la STAMICO na washiriki wa semina ya mazingira iliyofanyika wakati wa Tamasha la Nane la Biashara linaloendelea katika viwanja vya Maisara, Zanzibar.

Akiongea na washiriki wa semina hiyo,  Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Dkt. Venance Mwasse ambaye alikuwa mgeni rasmi amesema STAMICO iliona fursa katika taka ngumu  ambazo ni mabaki ya madini ya makaa ya mawe yanayochimbwa katika mgodi wake wa Kiwira na kuamua kuzalisha mkaa wa majumbani ili kuongeza nishati mbadala ya kupikia itakayosaidia kupunguza ukataji wa miti.

“Taka ngumu ni fursa ya kiuchumi, vijana wanatakiwa kutumia ubunifu ili waweze kushiriki katika shughuli mbalimbali za kiuchumi kwa kuwa wanapoamua kuwekeza katika taka ngumu itasaidia kutunza mazingira, kwa kuyafanya kuwa safi na rafiki kwa wananchi na wawekezaji”. Alisisitiza Mwasse

Ameongeza licha ya mkaa huo kuwa rafiki kwa mazingira bali umechangia kuongezeka kwa viwanda nchini kufuatia ununuzi wa mitambo ya uzalishaji mkaa huo, kutoa ajira na kuongeza pato la Taifa kupitia kodi na tozo mbalimbali.

Aidha ameipongeza TANTRADE kwa kuendelea kuboresha maonesho haya kwa kuandaa mafunzo na majadiliano mbalimbali yanayowakutanisha washiriki na wadau mbalimbali zikilenga kuleta uchumi jumuishi na endelevu wenye ubunifu kwa maslahi ya Taifa.

Awali Dkt. Mwasse alishiriki katika sherehe za maadhimisho ya  Mapinduzi ya Zanzibar katika uwanja wa Amani na baadaye kushiriki katika semina iliyoandaliwa na TANTRADE  na kutumia fursa hiyo kuwapongeza Wanzanzibar kwa kuendelea kuwa na moyo wa uzalendo katika kuyaenzi Mapindunzi Matukufu hususani siku ya Maadhimisho ya sherehe hizo za miaka 58 ya Mapinduzi ambazo zilifana sana.

Kwa upande wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara nchini (TANTRADE), Mkurugenzi Mkuu Bi Latifa  khamis amesema katika kutekeleza majukumu yake, Tantrade imekuwa mstari wa mbele katika  kuhakikisha mazingira yanalindwa na kutunzwa kwa kuwa mazingira ni kitu muhimu sana ni kitu muhimu na kila mtu anawajibu wa kuyatunza na kuyatumia mazingira kama fursa ya ajira katika kuwezesha biashara endelevu.

Ameipongeza STAMICO kwa kubuni bidhaa ambayo ni nishati mbadala inayolenga kutunza na kuhifadhi mazingira kwa kuwa sasa dunia ipo katika mpango kabambe wa kutunza mzingira ili kuzuia ongezeko la hewa ukaa ambayo ni hatari kwa mazingira.

Akitoa elimu kwa washiriki Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira Zanzibar (ZEMA) Bw.Sheha Mjaja Juma amesema mazingira ndio chanzo cha malighafi katika biashara, kwa kuwa kila kitu kinachozalishwa kwa ajili ya biashara kimetokea kwenye mazingira, hivyo ni jukumu la Serikali na mwananchi mmoja mmoja kuyalinda ili kutunza maliasili zilizomo kwa faida ya wananchi licha ya kuwa, hadi sasa Zanzibar ipo kwenye nafasi nzuri ya utunzaji wa mazingira. 

Amesema  kwa upande wa Zanzibar takribani hekta miatano za misitu hukatwa kila mwaka, hivyo katika kutunza misitu hiyo ni vyema wananchi wakazidisha matumizi ya nishati mbadala ambayo ni rafiki kwa mazingira, 

“asilimia 90 ni biomass ambayo ni kuni na mkaa hivyo kukiwa na nishati ambazo ni salama tutaokoa hekta 500 misitu kwa mwaka na mazingira yetu yataimarika kwa kuwa nishati mbadala ni muhimu sana katika kupunguza ukataji wa misitu”. 

Amesema ni vyema kuchukua taadhari ya kutunza mazingira kwa kuanza kutumia nishati mbadala ili kuhifadhi misitu na uoto wa asili  kwa kuwa kuendelea kukata miti kunaweza kupelekea mabadiliko ya hali ya hewa inayoweza kusababisha mvua kubwa kunyesha kwa wakati mmoja na kuleta mafuriko. 

Ametoa shime kwa wananchi kuchangamkia fursa mbalimbali zinazosaidia kutunza na kuhifadhi mazingira na kuachana na shughuli mbalimbali zinazoweza kuharibu mazingira zikiwemo ukataji wa miti kwa ajili ya nishati ya kupikia.

Kwa upande wa washiriki Bi Salima Othmary Amefurahishwa na semina hiyo ya mazingira ambayo imewafungulia fursa ambazo hawakuwahi kufikiria, hususani katika mawanda ya taka ngumu kwamba yanaweza kutoa fursa za kibiashara.

STAMICO imeendelea kushirikiana na TANTRADE katika kuendesha biashara mbalimbali kwa kuwa TANTRADE imekuwa kinara katika kutafuta fursa za kibiashara na kuwakutanisha wafanya biashara na Taasisi, Kampuni na watu binafsi ili kuimarisha mazingira ya biashara endelevu kwa manufaa ya Taifa.

Previous articleTUME YA MADINI YATOA BEI ELEKEZI KWA KWA BAADHI YA MADINI YANAYOZALISHWA NCHINI.
Next articleSERIKALI YAPOKEA DAWA ZA MINYOO NA VIRUTUBISHO ZENYE THAMANI YA MIL. 341
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here