MKUU Kassim Majaliwa amesema maamuzi yaliyofanywa na Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kumkaribisha muwekezaji wa ujenzi wa kiwanda cha mbolea cha Itracom ni sahihi kwa maendeleo ya sekta ya kilimo nchini.
Amesema Serikali itasimamia ujenzi wa mradi huo ili kuhakikisha azma ya Mheshimiwa Rais Samia ya kuendeleza sekta ya kilimo inafikiwa kwa sababu changamoto kubwa iliyokuwa inawakabili wakulima wengi ni upatikanaji wa mbolea ambayo inakwenda kuwa historia.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumamosi, Januari 15, 2022) wakati akizungumza na uongozi na wafanyakazi wanaojenga kiwanda hicho katika eneo la Nala jijini Dodoma. “Serikali imedhamiria kuimarisha sekta ya kilimo ili Watanzania wanaoitegemea wapate mafanikio.”
Mheshimiwa ambaye leo alifanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi huo amesema ameridhishwa na kasi ya ujenzi wake na kwamba Serikali inataka kuona Watanzania wengi wananufaika na uwekezaji huo. Ujenzi wa kiwanda hicho umefikia asilimia 52.
“Ujenzi wa kiwanda hiki ni matokeo ya ziara ya Mheshimiwa Rais Samia nchini Burundi, lengo ni kuhakikisha tunazalisha mbolea hapa nchini badala ya kutegemea kuagiza nje kwa kiasi kikubwa. Kiwanda hiki kinatarajiwa kuzalisha tani laki 600,000 kwa mwaka,” amesema.