Home LOCAL MSISAFISHE MASIKIO KWA PAMBA, SIKIO HUJISAFISHA LENYEWE: DKT. BAZILIO

MSISAFISHE MASIKIO KWA PAMBA, SIKIO HUJISAFISHA LENYEWE: DKT. BAZILIO

Daktari Bingwa wa Pua,Koo na Masikio kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa-Tumbi Dkt. Jane Bazilio akimhudumia mmoja wa wananchi wa Tabora waliofika kupata huduma za kibingwa kwenye hospitali ya rufaa ya mkoa wa Tabora-Kitete.
Daktari Bingwa wa Macho kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa-Temeke Dkt. Annamary Stanislaus na Daktari bingwa Mathew Yinza wa Tumbi wakitayarisha kifaa tayari kwa kuwahudimia wananchi.
 
Dkt. Mathew Yinza kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa-Tumbi akimhudumia mtoto aliyefika kupata hudum a za kibingwa.imeelezwa kwamba wananchi kuacha kujinununia dawa za macho bila ya kupata ushauri wa daktari.
Dkt. Annamary Stanislaus akitoa huduma kwa wananchi wa Tabora ambapo amewashauri mtu anapopata shida ya kutokuona vizuri ni vyema kuwahi hospitali  aangaliwe na sio kila shida ya kutokuona inatibiwa na miwani.
Wananchi wa Mkoa wa Tabora wakiwa wanasubiri kuonana na madaktari bingwa waliopo hospitali ya rufaa ya mkoa wa Tabora-Kitete wakitoa huduma za kibingwa kwa siku tano.

– Wananchi wakatazwa kujinunulia dawa za kutibu macho bila kuonana na Daktari

Na. Catherine Sungura, Tabora

Wananchi wameshauriwa kutoingiza maji kwenye masikio wakati wa kuoga pia kutosafisha masikio yao kwa kutumia pamba za masikio kwani kwa kawaida sikio hujisafisha lenyewe.

Hayo yamebainishwa na Daktari Bingwa wa Pua, Koo na Masikio, Dkt. Jane Bazilio kutoka Hospitali ya rufaa ya Mkoa-Tumbi wakati wa kambi ya huduma za kibingwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Tabora-Kitete.

Dkt. Bazilio amesema kwamba kwa kawaida sikio huwa linajisafisha lenyewe hivyo mtu anapotumia pamba anakuwa anatoa nta iliyoko kwenye sikio ambayo kazi yake ni kulilinda sikio.

“Katika kambi hii tumewaona wagonjwa wengi wenye matatizo ya masikio na pua, wananchi wengi wanafikiri ile nta ni uchafu kutokana na rangi yake ile ya kahawia (brown) na kusema wanatoa uchafu ile sio uchafu ina kazi yake ya kulinda sikio, nta ile msiitoe ina utaratibu wake wa kutoka kwenye sikio”. Alisisitiza Dkt. Bazilio.

Aidha, amesema wagonjwa wengi waliowaona katika kambi hiyo wanakuwa na shida ya Fangasi masikioni ambayo husababishwa na unyevunyevu kwenye masikio na kuwataka wananchi wanapokuwa wanaoga wasiingize maji kwenye masikio yao.

Hata hivyo amewashauri wazazi na walezi kuwakataza watoto wasichezee vitu vigeni kama vile vigorori kwani wameona watoto wameweka vitu hivyo kwenye pua na masikioni pia kuacha kuwasafisha watoto wadogo kwa pamba kwani wanaposafisha nta ile inaweza kuingia kwenye sikio na kusababisha kuziba kwa sikio na hata kwa watu wazima pia.

Naye, Daktari Bingwa wa Macho kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa-Temeke Dkt. Annamary Stanislaus amewataka wananchi kuacha mara moja tabia ya kujinunulia dawa za kutibu macho bila ya kuonana na madakatari kwa ushauri zaidi.

Amesema kuwa matatizo ya macho yako mengi hivyo sio vizuri mtu anapopata shida ya macho kujitibia mwenyewe kwani mara nyingi huwezi kujua kitu gani unaumwa..

“Kuna watu wanapata shida ya macho na wanaenda kujinunulia dawa na kuweka kwenye macho, matokeo yake wanaharibu zaidi kumbe wananunua dawa ambazo zinaharibu macho na hadi wanapofika hospitalini macho yameshaharibika”.

Kuhusu mtoto wa Jicho Dkt. Annamary amewatoa hofu wananchi wenye matatizo ya uoni unaotokana na mtoto wa jicho kutokuogopa na kuondoa imani ya kwamba ukifanyiwa upasuaji hatoona tena bali mtoto wa jicho ni mojawapo wa upofu unaotibika.

Zaidi ya Madaktari Bingwa ishirini kutoka hospitali za rufaa za mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Dodoma wapo Hospitali ya rufaa ya mkoa wa Tabora-Kitete kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi wa mkoa huo kwa huduma za kibingwa kwa magonjwa ya upasuaji, mfumo wa mkojo, pua, koo na masikio, kinywa na meno, macho, mifupa, magonjwa ya kinamama na uzazi , magonjwa ya watoto pamoja na magonjwa ya tiba (kisukari, moyo, presha, vidonda vya tumbo na mengineyo) ambapo huduma hizo zinatarajiwa kumalizika siku ya ijumaa wiki hii.

Previous articleTPA YAPONGEZWA HUDUMA BORA BANDARI YA KILWA
Next articleSERIKALI YATOA TAHADHARI JUU YA UWEPO WA UGONJWA USIOJULIKANA MKOANI KAGERA
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here