NA: NAMNYAK KIVUYO, ARUSHA
Ikiwa Leo ni siku ya mwisho zoezi la utambuzi wa anwani za makazi unaoendelea katika tano za jiji la Arusha ili kuingia kwenye hatua nyingine ya uwekaji wa majira ya nukta(Code Net) Wananchi wa kata ya Themi mtaa wa Themi Mashariki wameiomba serika kuongeza kasi ili waweze kunufaika na mfumo huo utakarahisisha mambo mengi ikiwemo biashara zao.
Godfrey Mgwasa mkazi wa mtaa huo alisema kuwa kama walivyosikia malengo ya zoezi hilo ni kwa manufaa ya wananchi na nchi kwa ujumla ni vema ikafanyika kwa wakati na haraka inayotakiwa na kumaliza mapema ili matumizi ya mfumo huo yaanze ili kuwanufaisha wananchi.
“Serikali waongeze spidi kwani tumechelewa ukilinganisha na nchi nyingine zilizoendelea tunatamani matumizi ya mfumo huu ionekane mapema,” Alisema Mgwasa.
Magreth Ignatus ambaye pia ni mkazi wa kata hiyo alisema ameelewa kuwa zoezi hilo lina faida kubwa kwani baada ya kukamili wakiwa majumbani anaweza kuagiza bidhaa na zikamfikia bila shida yoyote.
“Kama Mimi kulingana na hii biashara yangu ya duka na mboga mboga na matunda naamini nitaweza kuagiza machingwa nyanya na bidhaa zingine na hii itanirahisishia mimi kuokoa muda lakini pia kufanya shughuli zingine za nyumbani wakati nasubiri mzigo niliouagiza ufike,” Alisema Bi Magreth.
Kwa upande wake mwenyekiti wa mtaa wa Themi Mashariki kata ya Themi Godfrey Mushi alisema kuwa tangu kuanza kwa zoezi hilo la utambuzi wa uwekaji anwani za makazi zoezi limeenda vizuri lakini pia zinapotokea changamoto ndogo ndogo wanazirekebisha na zoezi linaendelea kufikia lengo.
“Leo tunaenda vizuri zaidi kuliko jana na juzi kwasababu watu wengi wameelewa juu zoezi hili na wale ambao tunakuta hawapo tunazipa nyumba namba na kuwaachia majirani fomu kwaajili ya kutoa taarifa zao na baadae tutakuja kuzipitia,” Alisema Mushi.
Hata hivyo manufaa ya mfumo huo ni kurahisisha utoaji, upatikanaji na upelekaji wa huduma kwa wananchi au wateja, Kuongeza wa ukusanyaji mapato, kuongeza ajira, kuimarisha ulinzi na usalama, kurahisisha upatikanaji wa huduma majumbani pamoja na Kuimarisha biashara kwa njia ya mtandao.