Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene akizungumza na Watendaji wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya.
Watendaji wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya wakiwa katika kikao na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu (Hayupo kwenye picha).
Kamishina wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Jenerali Gerald Kusaya akimuonesha Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu (hayupo kwenye picha) muonekano katika picha wa Jengo la Mamlaka litakalojengwa Itega Mjini Dodoma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene ametoa wito kwa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Nchini kuongeza nguvu katika kutoa elimu kwa umma juu ya athari za dawa za kulevya kwa vijana na wanachi wote kwa ujumla.
Hayo ameyasema alipotembelea na kujionea eneo la Hekta saba ambalo linatarajiwa kujengwa jengo la Makao Makuu ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Kanda ya Kati, katika eneo la Itega Jijijni Dodoma leo tarehe 17/01/2023.
“lazima tuvunje ukimya na tuongeze udhibiti wa matumizi ya bangi, hatuwezi kudhibiti matumizi ya bangi kwa kutegemea mamlaka pekee yake lazima tuweke mfumo na uratibu kwa kuanza kudhibiti kuanzia ngazi ya kijiji, Kata na Wilaya.” Amesema Simbachawene.
Tufike mahali tuone tunauwa Taifa; Vitu vingi vinavyotokea kwenye familia, na matokeo ya ajabu ya unyanyasaji msukumo wake ni matumizi ya madawa ya kulevya na ukipata urahibu unashindwa kuisadia jamii, unashindwa kuwajibika kwenye familia unashindwa kufanya shughuli za uzalishaji mali.
Waziri Simbachawene, ameongeza kuwa aina mpya ya Urahibu wa kucheza Kamari (Kubeti) ambayo inawakumba watu wote, na ina madhara kama urahibu wa madawa ya kulevya, lazima tujipange.
Kila mmoja ni shahidi watu wanapokuwa wanafanya Kamari ya kubahatisha, kwenye michezo ya mpira, hata kufanya kazi hawawezi, muda wote ni kuangalia mkeka tuu(kubeti)
Aidha kuna umuhimu wa kuziunganisha kwa kuziimarisha Taasisi zetu hizi za Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe na Mamlaka wa Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kisera na kisheria ili ziweze kushirikiana vizuri katika utendaji wa kazi.
Naye Kamishna wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Jenerali Gerald Kusaya amesema katika Mwaka huu wa fedha serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu imeweza kupeleka Vyuo vya Ufundi warahibu walioachana na matumizi ya dawa za kulevya wapatao 245 wanaolipiwa ada zote na Ofisi ya Waziri Mkuu na kila mmoja amechagua kitu anachotaka kusoma ili watakapomaliza warudi mtaani na waweze kuanza kujitegemea na kujenga uchumi wa nchi.
Katika kuhitimisha ziara hiyo kamishna Jenerali Kusaya ameomba serikali kuwasaidia warahibu wanaohitimu mafunzo ya Ufundi stadi na stadi za kazi kupewa vitendea kazi vitakavyowasaidia pindi watakaporudi kwenye jamii yao
Jumla ya warahibu wapatao 12,800 wanatarajia kuhitimu mafunzo kutoka kwenye vyuo vya ufundi wakiwa na ujuzi wa stadi mbalimbali za kazi na kuweza kujitegemea na kujenga uchumi.