Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi kutoka Tume ya Kurekebisha Sheria, Wawakilishi wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na afya Tanzania(TUGHE)ngazi ya Taifa na Mkoa wakiwa katika picha ya pamoja baada ya ufunguzi wa kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT ) Tawi la Mbeya leo hii.
Wajumbe hao wakiwa katika picha ya pamoja.
Mgeni rasmi katika Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania Jaji Mstaafu January Henry Msoffe akihutubia wajumbe wakati wa ufunguzi wa kikako hicho kilichofanyika mkoani Mbeya Ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT). Kushoto ni Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Kurekebisha Sheria, Bwana Khalist Luanda.
Jaji Mstaafu January Msoffe (katikati) akisisitiza jambo kwenye kikao hicho.
Mjumbe wakifuatilia kikako hicho.
Mwakilishi wa Vijana Bw. Azizi Mbuni (kulia) na Anneth Lyatuu (kushoto) wakifuatilia wasilisho katika mkutano huo.
Jaji Mstaafu January Henry Msoffe akiendelea na hotuba kwa wajumbe waliohudhuria baraza la wafanyakazi.
Na Bashiri Salum, Mbeya | JAJI Mstaafu January Msoffe ameipongeza Menejimenti ya Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania kwa kutoa mafunzo ya maandalizi ya kustaafu ambayo yanalenga kumjengea Mtumishi uwezo wa kujiandaa kabla ya kustaafu.
Amewakumbusha watumishi kuanza maandalizi ya kustaafu mara tu baada ya kupata barua ya kuajiriwa ili kupunguza hofu zinazowakabili watumishi wengi wakati wa kustaafu na kuwasababishia maradhi.
Akizungumza leo wakati akifungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) Tawi la Mbeya, Jaji Msoffe alisema watumishi wengi wamekuwa wakipata maradhi mbalimbali yanayotokana na hofu ya kustaafu utumishi kwa sababu ya kutojiandaa kustaafu.
Akiyataja maradhi hayo Jaji Msoffe alisema wastaafu wengi wamekuwa wakikabiliwa na maradhi yatokanayo na shinikizo la damu, vidonda vya tumbo msongo wa mawazo na sonona ambapo amebainisha kuwa matatizo hayo yanaweza kupungua kwa kuanza ujasiriamali kabla ya kustaafu ili kuwa na kipato cha uhakika baada ya kustaafu.
“Nimetaarifiwa kwamba katika Baraza hili kutakuwa na mada mbambali ambazo zitatufundisha kujiandaa na maisha baada ya kustaafu ili kuepukana na maradhi yasiyo yalazima”.alisema.
Aidha, Jaji Msoffe aliiomba Menejimenti ya Tume ya Kurekebisha Sheria kuendelea kutoa elimu juu ya mabadiliko yanayosababishwa na mfumo mpya wa taarifa za utumishi na mishahara (New Humani Capital Management Information System) ili watumishi waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufasaha huku akiwataka kuwa tayari kupokea mabadiliko mbalimbali ya kiutumishi.
“Binadamu wote ni waoga wa mabadiliko ingawa katika hali halisi mabadiliko ni jambo lisiloepukika maishani, nilazima tuwe na utayari wakupokea mabadiliko hatakama hatuyapendi. Alisema Jaji Henry Msoffe.
Jaji Msoffe alitumia nafasi hiyo kuwakumbusha watumishi wote kushiriki kikamilifu katika zoezi la Sensa yaTaifa ya Watu na Makazi itakayofanyika baadaye mwaka huu ili kuisaidia Serikali kupata idadi sahihi ya watu waliopo katika maeneo ya kiutawala au kijographia.
Awali Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania Bw. Khalist Luanda akitoa maelezo ya awali alisema kikao hicho ni cha 17 ambapo Tume imeendelea kutekeleza majukumu yake ya kisheria.
Bw. Luanda alisema katika kikao hicho wajumbe watakuwa na fursa ya kujifunza masula mbalimbali ikiwa ni pamoja na ujasiriamali, maandalizi ya maisha baada ya kustaafu na mfumo mpya wa taarifa za kiutumishi na mishahara.
Alisema masuala hayo yatawasaidia watumishi kuongeza uelewa kuhusu utendaji wao wa kazi wa kila siku na kuboresha maisha yao wakiwa kazini na baada ya kustaafu
Akitoa maelezo ya bajeti ya mwaka 2021/2022 kwa mwaka huu Bw. Luanda alisema Tume ilitengewa bajeti ya Sh. Bilion 3.24 ambazo kiasi cha Sh. Milioni 820.9 ikiwa ni mishahara na Sh. Bilion 2.42 ikiwa ni kwa ajili ya matumizi mengine.
Aidha Katibu Mtendaji huyo akabainisha kwamba Tume tayari imetekeleza baadhi ya majukumu yake iliyojiwekea kwa mwaka wa fedha 2021/2022 ikiwemo ununuzi wa magari manne (4) ambapo tayari mawili yameshawasili Ofisi yaTume.
Akimalizia maelezo yake ya awali Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume alifafanua kwamba kwa Mwaka wa Fedha 2022/23 mwelekeo wa bajeti ya Tume ya kurekebisha Sheria Tanzania ni kutumia kiasi cha Sh.Bilioni 3.206 ambapo kati ya fedha hizo Sh. milioni 782.62 ni kwa ajili ya mishahara na Sh. Bilioni 2.424 ni kwa ajili ya matumizi mengine.
Baraza hilo lilihudhuriwa na wajumbe kutoka Tume ya Kurekebisha Sheria, Wawakilishi wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na afya Tanzania (TUGHE) ngazi ya Taifa na Mkoa.