Na.WAF,Bunda
Vituo vya Afya na Zahanati nchini vimetakiwa kuboresha usimamizi wa miongozo na kufufua kamati za huduma za afya.
Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi wakati wa ziara yake katika Halmashauri ya Bunda
Akiongea na watumishi wa vituo hivyo kwa nyakati tofauti Katibu Mkuu huyo alisema wamekuta vituo hivyo vinatoa huduma za afya kama kawaida ila kuna mapungufu kwenye eneo la usimamizi wa miongozo kama ile ya utunzaji wa takwimu za utoaji dawa zinazokosekana, wagonjwa wanaopata misamaha, uwajibikaji kwa Kamati za Dawa (Therapeutic Commitees).
Aidha Katibu Mkuu amebaini udhaifu wa kutokuwepo kwa Kamati za Afya za vijiji za kusimamia Zahanati na vituo ya afya.
Akitolea mfano Prof. Makubi alibaini hakuna rejista ya kuonyesha mgonjwa yupi kakosa dawa au vipimo na gharama ya kiasi gani Mwananchi kasamehewa.
Katika hali ya kushangaza kwenye vituo hivyo pia amekuta hawafanyai kazi kwa mfumo wa TEHAMA (GOTHOMIS) wa huduma na upokeaji malipo zinazotolewa hali inayosababisha upotevu mkubwa wa fedha za umma kwenye vituo hivyo.
“Serikali imeweka mfumo wa ukusanyaji wa malipo katika ofisi zake ikiwamo vituo vya afya,kwa kutotumia mfumo huo inasababisha kupotea na mapato yanayokusanywa na hivyo kusababisha usumbufu wa utoaji huduma bora kwa wananchi.
Hata hivyo Prof. Makubi alielekeza vituo hivyo kuunda kamati za huduma za afya ili ziweze kusaidia kupitisha mipango na kusimamia rasilimali zinazopokelewa na kutolewa za bidhaa za dawa,vifaa na vifaa tiba pamoja na shughuli zote za uwakilishi wa wananchi katika vituo vya afya.
Aidha, Katibu Mkuu amebaini Kamati za Huduma za Afya za Mikoa na Wilaya, zinashindwa kufanya usimamizi wa matokeo au kubaini changamoto na kuzitatua haraka.
Katibu Mkuu ameelekeza Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya kubadilika katika usimamizi ili kutatua kero na kuleta matokeo ya ubora wa huduma na utunzaji takwimu .
Vile vile, Katibu Mkuu huyo ameagiza watoa huduma wa vituo hivyo kutoa elimu kuhusu Magonjwa Yasiyoambukiza kwa wananchi wanaofika kupata huduma za afya pamoja na kufanya kazi kwa weledi na nidhamu ikiwemo lugha nzuri.