Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali akitazama mita zinazoonesha ujazo wa gesi inayoingia kwenye magari yanayotumia gesi katika kiwanda cha kuzalisha Saruji cha Dangote, wakati wa ziara ya kukagua miundombinu ya usambazaji wa gesi ya kupikia majumbani, Aprili 1, 2022, mkoani Mtwara.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali (kushoto) na Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Dunstan Kyobya wakibadilishana mawazo, wakati wa ziara ya kukagua miundombinu ya usambazaji wa gesi ya kupikia majumbani, Aprili 1, 2022, mkoani Mtwara.
Na: Zuena Msuya, Mtwara.
Imeelezwa kuwa Serikali inaendelea na usambazaji wa miundombinu ya kusambaza Gesi asilia kwa matumizi ya kupikia majumbani na katika Taasisi mbalimbali zinazotoa huduma ya chakula kwa watu wake.
Hayo yameelezwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali wakati wa ziara yake ya kukagua usambazaji wa miundombinu ya Gesi asilia kwa matumizi ya kupikia majumbani na katika Taasisi zinazotoa huduma ya chakula kama vile Shule na Magereza. Ziara hiyo ameifanya Aprili 1, 2022 mkoani Mtwara.
Katika ziara hiyo, Mahimbali ametembelea baadhi ya Taasisi zinazotumia gesi asilia kwa ajili ya kupikia Gereza la Lilungu, Shule ya Sekondari ya Mtwara pamoja na baadhi ya nyumba za wakazi wa Mtwara ambao tayari wameunganishwa na kutumia huduma hiyo.
Naibu Katibu Mkuu huyo ametoa wito kwa wakazi wa Mtwara na maeneo yanayopitiwa na miundombinu ya gesi kuchangamkia fursa hiyo kwa kuwa ni gharama nafuu ikilinganishwa na nishati nyingine ya kupikia.
Vilevile ametembelea na kukagua Miundombinu ya kiwanda cha kuchakata gesi asilia cha Madimba pamoja,visima vya gesi vya vilivyopo eneo la Mnazi bay pamoja kiwanda cha kuzalisha Saruji cha Dangote.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Dunstan Kyobya aliwataka wawekezaji wa ndani wakiwemo wakazi wa Mtwara na nje ya Nchi, kuwekeza katika mkoa huo kwa kuwa una nishati ya gesi ya kutosha.
Kyobya alishauri Taasisi zinazohusika na nishati hiyo, kuongeza kasi ya kutoa huduma ya kusambaza gesi hiyo majumbani na katika taasisi zinatoa huduma ya chakula nchini ili kupunguza gharama za uendeshaji na kutunza mazingira.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na kampuni tanzu inayosimamia miundombinu ya gesi (GASCO) ya Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC), ni kuwa, wateja 425 katika mkoa huo wa Mtwara wameunganishwa na kutumia gesi asilia kwa ajili ya kupikia.
Wakizungumza wakati wa ziara hiyo, Mkuu wa Gereza la Lilungu Joseph Sabayo, pamoja na Mkuu wa Shule ya Sekondari Mtwara, Riyadh Kadhi wameishukuru Serikali kwa kuunganishiwa gesi asilia ya kupikia katika taasisi zao na kusema kuwa gesi hiyo imesaidia kupunguza gharama za matumizi ya fedha zilizokuwa zikitumika kununua kuni.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Shule ya Sekondari Mtwara, Riyadhi Kadhi, ni kuwa kwa Sasa wanatumia shilingi Milioni 1.4 kwa mwezi kwa ajili ya kununua gesi ya kupikia shuleni hapo, ambapo awali walikuwa wakitumia shilingi Milioni Tatu mpaka Nne kwa ajili ya kununua kuni. Hivyo Gesi hiyo imeokoa takribani shilingi Milioni Mbili zilizokuwa zikitumika kununua kuni.
Kadhi alisema kuwa matumizi ya Gesi pia yamerahisisha na kupunguza muda wa kuandaa chakula kwa wanafunzi wa shule hiyo na pia imeweka mazingira rafiki kwa wapishi wanapotekeleza majukumu yao.