Na: Stella Kessy, DAR.
Afisa Michezo wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Allen Alex amewataka viongozi wapya wa Shirikisho la Michezo ya Mashirika ya Umma,Taasisi na Makampuni Binafsi (SHIMMUTA) kurekebisha mapungufu yote yaliopo, kwa maendeleo ya Shirikisho pamoja na michezo nchini.
Hayo ameyasema leo tarehe 9 Aprili, 2022 baada ya kukamilika kwa uchaguzi wa viongozi wa Shirikisho hilo uliofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP) Jijini Dodoma.
“Kwanza kabisa nawapongeza kwa kuaminiwa na wajumbe kuweza kuwachagua kama viongozi wao, sasa mnapaswa kuwatumikia kwa juhudi zote, lakini pia mmeona kuna baadhi ya mapungufu yaliopo katika sehemu chache kwenye Shirikisho lenu, kwa mfano bado katiba yenu mnahitaji kuendelea kuiboresha ndani ya muda mfupi, ili kuendana na kasi mnayohitaji” amesema Allen.
Kwa upande wake rais mpya wa SHIMMUTA, Roselyne Massam amewahakikishia wajumbe waliomwamini na kumchagua, kuwa atashirikiana na watu wote ili kutimiza malengo yaliyowekwa na maagizo yaliyotolewa na uongozi wa BMT.