NAIBU Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amebainisha kuwa Serikali imetenga kiasi cha shilingi Bilioni 200 kwaajili ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba katika mwaka wa fedha 2022/2023 huku Bilioni 74.3 zikiwa tayari zimetolewa katika kumaliza changamoto ya upungufu wa dawa na vifaa tiba nchini.
Dkt. Mollel amesema hayo leo Novemba 11,2022 wakati akijibu swali la Mhe. Ghati Zephania Chomete, Mbunge wa viti maalumu katika kikao cha kumi cha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jijini Dodoma.
Amesema, Serikali ya awamu ya sita imedhamiria kutatua changamoto za huduma za afya kwa wananchi, huku kiasi cha shilingi Bilioni 74.3 zikiwa tayari zimetolewa kati ya Bilioni 200 zilizotengwa katika mwaka wa fedha 2022/2023 kwaajili ya ununuzi wa dawa pamoja na vifaa tiba.
“Katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali imetenga bajeti ya shilingi Bilioni 200 kwa ajili ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba na hadi kufikia tarehe 30 Oktoba, 2022 Serikali imekwisha toa jumla ya shilingi bilioni 74.3 kwa ajili ya manunuzi ya dawa na vifaa tiba ili kuimarisha upatikanaji wake katika ngazi zote za utoaji wa huduma za Afya.” Amesema Dkt. Mollel.
Aidha, amesisitiza kuwa, Serikali itaendelea kuboresha na kuimarisha upatikanaji wa huduma za Afya nchini kwa kuboresha miundombinu ikiwemo kuweka vifaa tiba vya kisasa, kuajiri Wataalamu wa Afya pamoja na kuwapandisha madaraja ili kuongeza morali ya kuendelea kutoa huduma kwa wananchi.
Akijibu swali la nyongeza Dkt. Mollel amesema, Serikali imepeleka vifaa vyenye thamani ya shilingi Bilioni 3 katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara – Kwangwa vitavyosaidia kutatua changamoto ya wananchi kwenda mikoa ya mbali kutafuta huduma hizo.
Ameendelea kusema kuwa, ifikapo Desemba 12, 2022 hospitali hiyo itaanza kutoa huduma zote, huku akisisitiza tayari CT-SCAN imeshafungwa na MRI ikisubiri chumba kikamilike ili huduma hiyo nayo ianze kuwanufaisha wananchi wa Mkoa wa Mara na nchi za jirani.
Sambamba na hilo, Dkt. Mollel amesema, Serikali imejipanga katika udhibiti wa dawa kwa kutengeneza mfumo mzuri kutoka zinapotoka ngazi ya taifa mpaka zinapofika katika kituo husika, huku akisisitiza ushirikiano baina ya viongozi, kamati za afya na wananchi katika kusimamia dawa ili ziweze kuwafikia walengwa.
Pia, ameelekeza hospitali kutumia mapato ya ndani kutatua changamoto za dawa endapo zitajitokeza ili kutatua changamoto hizo kwa wagonjwa wanaoenda kupata huduma katika maeneo hayo ya kutolea huduma.