Na: Maiko Luoga Tanga
Wakristo nchini wametakiwa kujenga tabia ya kuwatembelea, kuwafariji na kutoa sadaka zao kwa wahitaji wakiwemo watoto yatima na makundi ya watu wenye mahitaji maalumu ambao hutegemea jamii ili waweze kuishi.
Wito huo umetolewa April 17, 2022 na Askofu Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania na Dayosisi ya Tanga Maimbo Mndolwa, wakati akihubiri kwenye misa ya Pasaka iliyofanyika katika Kanisa Anglikana Mtakatifu Anna Muheza Dayosisi ya Tanga.
Pamoja na ratiba za kawaida za Pasaka Misa hiyo ilikuwa na lengo la kutoa faraja na matendo ya huruma kwa Watoto na vijana wenye mahitaji maalumu wanaotunzwa na Kituo cha Faraja Muheza (Muheza Hospice Care) kilichopo chini ya Kanisa Anglikana Tanzania Dayosisi ya Tanga.
“Wakati ukifurahi wewe na watoto wako kumbuka wapo wengine wanahitaji hiyo furaha lakini wameikosa, hawa hawakupenda kuwa hivi lakini ni mapenzi ya Mungu maana hapa wengine wamepoteza wazazi wao kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ajali ambazo hata mimi na wewe zinaweza kutukuta leo na kuacha watoto wetu kama walivyo hawa” Askofu Mndolwa.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Muheza Hospice Care Bw, Edgar Ngelangela amesema Kituo hicho kilianzishwa rasmi mwaka 2001 na kusajiliwa mwaka 2002 na wizara ya mambo ya ndani ya nchi kama asasi ya kiraia yenye lengo la kutoa huduma za tiba shufaa kwa wagonjwa wenye magonjwa ya kusendeka kupitia wataalamu wa Afya wanaotembelea wagonjwa majumbani na wale waliolazwa Hospital.
“Mwaka 2022 tunajumla ya akina mama 77 wenye magonjwa 71 wamejifungua watoto ambao wapo salama hakuna mwenye maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, Klabu ya Watoto na Vijana rika inajumla ya watoto na vijana 371 wavulana 164 na wasichana 107 ambao wanaendelea kuhudumiwa na Kituo.
Baadhi ya wadau na waumini walioungana na Askofu Maimbo Mndolwa kushiriki Ibada hiyo walijitokeza na kutoa mahitaji mbalimbali ya majumbani na shuleni ikiwemo vyakula, mavazi na vifaa vya masomo ili kuwawezesha Watoto na Vijana hao kupata furaha kama walivyo wengine katika jamii.
Mwisho.
Kwa kulinda utu wa watoto husika icha zao zimehifadhiwa.