Na: Englibert Kayombo – WAF, Bungeni, Dodoma.
Katika kuboresha zaidi huduma za afya kwa Wazee, Serikali Mwaka huu wa fedha 2022/2023 imepitisha Muundo mpya ambao umewezesha Wizara kuanzisha seksheni ndani ya kurugenzi ya Tiba inayoshughulika na Huduma za Afya ya Wazee (Geriatrics), Huduma za Utengamao (Rehabilitation services) na Huduma za Tiba Shufaa (Palliative Therapy).
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya Mheshimiwa Ummy Mwalimu leo alipokuwa akijibu swali lililoulizwa na Mheshimiwa Shabani Shekilindi (Mbunge) kuhusu mpango wa Serikali kuboresha Huduma za Afya kwa Wazee badala ya kutumia dirisha la Wazeen ambalo limekuwa likileta usumbufu kwa Wazee.
“Serikali inaendelea kuimarisha huduma za afya za wazee. Kwa miaka mingi wazee wamekuwa wakipatiwa huduma mahsusi kwa kupitia madirisha maalum ya huduma za afya kwa wazee yaliyotengwa katika vituo vya kutolea huduma” amesema Waziri Ummy Mwalimu.
Amesema chini ya Seksheni hiyo Uratibu wa huduma au afua mbalimbali za afya ya wazee utafanyika na maboresho ya huduma za afya kwa wazee yatapokelewa na kuchakatwa na kupatiwa majawabu kwa wakati.
“Rasimu ya mwongozo wa utekelezaji wa mkakati wa huduma za afya kwa wazee ipo katika ngazi ya maboresho hivi sasa. Uzee na kuzeeka havikwepeki, Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea Kuwaenzi Wazee Wetu” amesema Waziri Ummy Mwalimu.
Waziri Ummy amesema yapo mapungufu katika utoaji wa huduma kwenye Dirisha la Wazee na kutoa mapendekezo ya kubadilishwa mfumo wa utoaji wa huduma hizo kwa Wazee kutoka kwenye madirisha ya wazee kwenda kwenye Bima ya Afya kwa wote ili kuwawezesha wazee hao wanakuwa na uhakika wa matibabu bila vikwazo.
“Wazee wengi sasa hivi wanakwenda kwenye Dirisha la Wazee hakuna dawa, wakiwa na Bima tunaamini watapata huduma na kupata dawa” amesema Waziri Ummy Mwalimu.