Asisitiza Serikali kuendelea kuwekeza katika elimu inayojenga ujuzi na maarifa
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba leo Januari 05, 2026 amezindua Skuli ya Sekondari ya Chukwani na kutumia fursa hiyo kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa maboresho makubwa aliyoyafanya katika sekta mbalimbali ikiwemo ya elimu.
“Ninampongeza Dkt. Mwinyi kwa ujenzi wa skuli hizi za kisasa zenye vifaa bora na zilizozingatia matumizi bora ya ardhi kwa ujenzi wa skuli za ghorofa. Elimu ndio urithi sahihi, watoto someni kwa bidii na mtumie vizuri fursa hii ambayo Serikali imewapatia. Hakikisheni mnaitunza vizuri miundombinu hii.”
Waziri Mkuu amezindua rasmi Skuli hiyo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maadhimisho ya miaka 62 ya Mapinduzi kwa vitendo, ambapo amesema kuwa wakiweka kipaumbele katika maendeleo ya sekta ya elimu vijana wa Kitanzania wataweza kujikwamua kiuchumi.
“Ujenzi wa Skuli hii ya Sekondari ya Chukwani ni mwendelezo wa azma ya Serikali ya kujenga skuli za kisasa zinazokidhi mahitaji ya mtaala mpya. Skuli hii ninayofungua leo imejengwa kwa viwango vya kisasa, ikiwa na Maabara za Sayansi na Kompyuta, Maktaba na Vyumba vya Madarasa vinavyowezesha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika kufundishia na kujifunzia.”
Pia, Mheshimiwa Waziri Mkuu amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuwekeza katika elimu inayojenga umahiri, ujuzi na maadili ili kuwaandaa vijana wenye uwezo wa kufikiri, kubuni na kufanya kazi kwa vitendo.
Amesema maandalizi yanayofanywa kwa vijana hao si kwa ajili ya mitihani pekee bali kwa kukabiliana na maisha, soko la ajira na kuchangia maendeleo ya Taifa, hivyo Serikali itaendelea na ujenzi wa skuli za kisasa na utekelezaji wa mtaala mpya pamoja na kuimarisha maandalizi ya walimu na mapitio ya mitaala ili elimu bora ilete tija halisi kwa Taifa.
Mheshimiwa Dkt. Mwigulu ametoa wito kwa wananchi, walimu na wanafunzi kwa pamoja waweke kipaumbele katika kulinda, kutunza na kutumia ipasavyo miundombinu ya elimu iliyowekezwa kwa gharama kubwa, kwani ni mali ya umma na urithi wa vizazi vya sasa na vijavyo.
Pia, Waziri Mkuu amewasihi wazazi na Watanzania kwa ujumla, wajitahidi kulibeba kwa pamoja jukumu la malezi ya vijana. “Jukumu hili la malezi huanzia nyumbani, ndipo hufikishwa shuleni kwa walimu. Jukumu hili si la walimu pekee, bali ni jukumu letu sote kama jamii.”
Kaulimbiu ya maadhimisho hayo inasema: “Amani na Umoja ndiyo Msingi wa Maendeleo Yetu”, ambapo Waziri Mkuu amesema inaakisi ukweli wa msingi kwamba maendeleo ya Taifa lolote hayawezi kupatikana bila kuwepo kwa amani, utulivu na mshikamano wa wananchi wake.
Amesema kaulimbiu hiyo inawakumbusha wananchi kuwa mafanikio yote wanayoyaona leo, ikiwemo uwekezaji mkubwa katika elimu na miundombinu ya kijamii, yamewezekana kwa sababu ya mazingira ya amani. “Ndugu Wananchi; umuhimu wa kaulimbiu hii uko katika kuhamasisha jamii kuendelea kuilinda na kuienzi amani, kuimarisha umoja wa kitaifa na kushiriki kwa pamoja katika ujenzi wa Taifa”.
Naye, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Khadija Salum Ali amesema kuwa Serikali imejipanga kuendeleza ujenzi wa skuli za kisasa zinazotumia TEHAMA ili kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia. “TEHAMA inamuwezesha mwalimu aliye popote kuweza kufundisha wanafunzi.”
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Khamisi Abdallah Said amesema mradi huo unaohusisha ujenzi miundombinu mbalimbali ikiwemo vyumba vya madarasa 42, ofisi za walimu, maabara na chumba cha kompyuta umegharimu shilingi bilioni 6.1 na ulianza Mei 2025 hadi Desemba 2025.
Awali, baadhi ya wanafunzi wa skuli hiyo akiwemo Shekha Hababuu Makame wa kidato cha pili wameishukuru Serikali kwa ujenzi wa miundombinu hiyo ambayo itawaongezea ujuzi na maarifa, hivyo wameahidi kutoiangusha na badala yake watasoma kwa bidii na maarifa.





