Home LOCAL SERIKALI YAENDELEA KURASIMISHA UJUZI WA VIJANA – Prof. MKENDA

SERIKALI YAENDELEA KURASIMISHA UJUZI WA VIJANA – Prof. MKENDA

Na Lilian Ekonga………….

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema Serikali inaendelea kuimarisha utaratibu wa kurasimisha ujuzi wa vijana waliopata stadi mbalimbali nje ya mfumo rasmi wa elimu, ili kuwawezesha kutambulika rasmi na kupata vyeti vinavyotolewa na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA).

Akizungumza leo, Desemba 10, 2025, jijini Dar es Salaam, Prof. Mkenda amesema mpango huo unalenga kufungua fursa zaidi za ajira kwa vijana kupitia tathmini ya kazi wanazozifanya na kuwapatia vyeti baada ya wataalamu wa VETA kupima kiwango cha ujuzi wao.

“Kuna utaratibu tumekuwa tukiufanya, na tunaendelea kuuimarisha wa kurasimisha ujuzi ulio mitaani. Ukifika VETA, wataalamu watakupima, na baada ya hapo utapata cheti kitakachokuwezesha kupata kazi,” amesema Prof. Mkenda.

Ameeleza kuwa juhudi hizo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kujenga nguvu kazi yenye ujuzi wa vitendo, ambayo inaweza kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya kiuchumi, hasa kupitia sekta za viwanda, sayansi na teknolojia.

Alikadhalika Prof. Mkenda pia amebainisha kuwa ili taifa liweze kupiga hatua kubwa za maendeleo, ni lazima uwekezaji mkubwa ufanyike katika masomo ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu. Amesema Serikali imeweka kipaumbele maalum katika kuimarisha elimu hiyo kwa ngazi zote.

“Kuna msisitizo mkubwa sana umewekwa kwenye masomo ya sayansi. Kwa mfano, chini ya maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kila mkoa umejengewa Sekondari ya Wasichana ya Sayansi,” amesema Prof. Mkenda.

Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuhakikisha vijana wote wenye uwezo wa kusoma masomo ya sayansi wanasomeshwa kwa gharama za Serikali, ili kuhakikisha hakuna anayekatishwa tamaa kutokana na changamoto za kifedha.

Sambamba na hayo Waziri amesema Serikali imeanzisha Tuzo Maalumu ya “Mwalimu Nyerere”, shindano la uandishi litakalowawezesha vijana kushindana, ambapo washindi watapata msaada wa kifedha na fursa za kuuza kazi zao katika maeneo mbalimbali.

Aidha, amesema Serikali inaendelea kuimarisha ushirikiano kati ya vyuo na maeneo ya uzalishaji ili kuongeza nafasi za mafunzo kwa vitendo kwa vijana, akitolea mfano makubaliano ambayo tayari VETA imesaini kwa ajili ya kuwaunganisha vijana wenye ujuzi na sekta ya uzalishaji moja kwa moja.

Prof. Mkenda amehitimisha kwa kusisitiza kuwa hatua hizo zote ni sehemu ya dhamira ya Serikali ya kujenga taifa lenye wataalamu wabunifu na wenye ujuzi halisi, watakaoharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii kupitia matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu.

 http://SERIKALI YAENDELEA KURASIMISHA UJUZI WA VIJANA – Prof. MKENDA