Home LOCAL NHC YAUNGA MKONO MAENDELEO YA UNUNUZI NA UGAVI KUPITIA KONGAMANO LA TAIFA

NHC YAUNGA MKONO MAENDELEO YA UNUNUZI NA UGAVI KUPITIA KONGAMANO LA TAIFA

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

ARUSHA

Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) linashiriki katika Kongamano la 16 la Mwaka la Wataalam wa Ununuzi na Ugavi jijini Arusha.

Kongamano hilo ambalo limeanza leo Desemba 19,2025 linfanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC) ambapo mgeni rasmi ni Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Balozi Khamis Mussa Omar ambaye amewakilishwa na Naibu Waziri, Mhandisi Mshamu Ali Munde.

Aidha,kongamano hilo linawakutanisha pamoja wadau mbalimbali wa sekta ya ununuzi na ugavi.

Katika kongamano hilo, NHC ni miongoni mwa wadhamini, jambo linalodhihirisha dhamira ya shirika hilo katika kuunga mkono maendeleo ya taaluma ya ununuzi na usimamizi wa mnyororo wa ugavi nchini.

Kongamano linaongozwa na kauli mbiu isemayo: “Kujenga wataalamu kwa ajili ya usimamizi wa mnyororo wa ugavi wa siku zijazo: Ujuzi wa uongozi na ubunifu”, kauli mbiu inayolingana kikamilifu na mwelekeo wa kimkakati wa NHC katika utekelezaji wa miradi ya makazi.

Ushiriki wa NHC katika mikutano na makongamano ya kitaaluma kama hili umeendelea kuleta matokeo chanya katika kuimarisha sekta ya makazi nchini.

Kupitia majukwaa haya, NHC hupata fursa ya kubadilishana uzoefu, maarifa na mbinu bora za usimamizi wa ununuzi na ugavi, hali inayochangia kuboresha ufanisi wa utekelezaji wa miradi ya nyumba, kupunguza gharama, na kuongeza ubora wa huduma zinazotolewa kwa wananchi.

Vilevile, makongamano haya huchochea ubunifu, matumizi ya teknolojia za kisasa, pamoja na uimarishaji wa uongozi katika usimamizi wa rasilimali, mambo ambayo ni muhimu katika kukabiliana na changamoto za ongezeko la mahitaji ya makazi nchini.

Ushiriki wa NHC pia huimarisha ushirikiano na wadau wa sekta binafsi na taasisi za kitaaluma, hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo endelevu ya sekta ya makazi na uchumi wa Taifa kwa ujumla.