Home LOCAL MHE.KAPINGA AZIHIMIZA KAMPUNI KUHUISHA TAARIFA KWA MSAJILI WA KAMPUNI 

MHE.KAPINGA AZIHIMIZA KAMPUNI KUHUISHA TAARIFA KWA MSAJILI WA KAMPUNI 

Mheshimiwa Judith Kapinga, Waziri wa Viwanda na Biashara amezihimiza  kampuni zinazofanya biashara nchini kuendelea kuhuisha taarifa zao kwa Msajili wa Kampuni ili zisaidie kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara nchini, mifumo ya usajili na utoaji wa leseni, sheria zinazosimamiwa na  Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) na kuweza kushirikiana na Taasisi nyingine hususan Mamlaka za serikali za mitaa na mamlaka za udhibiti kwa kuunganisha mifumo ya utoaji huduma ili kuondoa urasimu wa utoaji huduma kwa wateja.
Wito huo umetolewa leo tarehe 18 Desemba, 2025 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari juu ya utekelezaji wa majukumu ya wizara ya viwanda na biashara katika ofisi za idara ya habari-MAELEZO jijini Dar es Salaam.
Mhe Kapinga ameeleza kuwa taasisi ya BRELA iliyochini ya Wizara yake imefanikiwa na inaendelea kuunganisha mifumo yake na mifumo ya Taasisi nyingine ambapo Mfumo wa Usajili kwa njia ya Mtandao (ORS) umeunganishwa na jumla ya Taasisi 29 za Serikali na Binafsi ili kurahisisha upatikanaji wa Taarifa zinazotumiwa na Taasisi hizo kwa hatua mbalimbali za utekelezaji wa majukumu ya Taasisi hizo.
 “Tumeboresha mifumo ya kielektroniki ya Usajili na Leseni ambapo huduma zote za usajili na utoaji Leseni unafanyika kwa njia ya mtandao kupitia mifumo ya kieletroniki [Online Registration System (ORS), Tanzania National Business Portal (TNBP) na Beneficial Ownership Portal (BO)] ambapo matumizi ya mifumo hiyo imeendelea kurahisha utoaji wa huduma na kuwafikia wadau kwa haraka” amesisitiza Mhe Kapinga.
Mhe Kapinga amesisitiza kwa kusema kuwa Tanzania ya viwanda haiwezi kujengwa bila vijana. Serikali imeweka misingi, imejenga miundombinu, imefungua masoko, imerahisisha mikopo, imerahisisha usajili wa biashara sasa ni jukmu la vijana kuchukua hatua ambapo Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Tanzania umedhamiria kuwashika mkono kila hatua ya safari hii muhimu ya maendeleo ya vijana na Taifa kwa ujumla.
Kwa kipindi cha miaka minne iliyopita BRELA imeongeza idadi ya Sajili na Leseni kwa kusajili kampuni kutoka 9630 hadi 23,365, majina ya biashara 17,200 hadi 31,123, alama za biashara na huduma kutoka 2,406 hadi 3,148, leseni za biashara kundi A kutoka 11,726 hadi 22,718, leseni za viwanda kutoka 236 hadi 991 na utoaji wa hataza kutoka 36 hadi 76 ongezeko la takwimu hizi ni kwa mwaka ambapo ukuaji huu ni kutoka na maboresho ya utoaji wa huduma na maboresho ya mazingira ya ufanyaji biashara nchini.