Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Patrobas Katambi, ameitaka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) kuimarisha utoaji wa elimu kwa umma ili kufikisha taarifa kwa Watanzania, hususan vijana, kuhusu namna ya kurasimisha biashara zao na kupata leseni za biashara.
Mhe. Katambi ametoa maelekezo hayo leo, tarehe 18 Desemba, wakati wa ziara yake katika ofisi za BRELA alipokutana na Menejimenti ya Wakala, ambapo alieleza kuwa kwa sasa Serikali imeelekeza nguvu kubwa katika kuwawezesha vijana.
“Katika usajili wa kampuni na maeneo ya biashara, suala la elimu ni muhimu zaidi na linapaswa kupewa kipaumbele. Ni muhimu kuhakikisha taarifa zinawafikia Watanzania kuhusu mabadiliko yanayotokea, huduma mpya zinazoanzishwa pamoja na maeneo yanayowakwaza zaidi wafanyabiashara katika usajili, ili yapatiwe ufumbuzi na elimu itolewe ipasavyo,” amesema Mhe. Katambi.
Aidha, ameongeza kuwa Serikali imetenga asilimia 30 ya tenda zote zinazotolewa kwa ajili ya kampuni zinazomilikiwa na vijana, pamoja na kuwepo kwa mfumo wa mikopo ya asilimia 10 katika kila Halmashauri kwa ajili ya vijana.
Kutokana na fursa hizo, vijana wengi wamekuwa wakifungua kampuni na kujiunga katika vikundi mbalimbali. Endapo watapatiwa msaada, uratibu na ushauri sahihi kutoka BRELA, wataweza kujiimarisha kibiashara, kurasimisha biashara zao na kuchangia pato la taifa kwa kuwa vijana wengi wamejikita katika sekta ya kilimo wataweza kujihusisha na kilimo-biashara.
Katika utekelezaji wa hayo, Mhe. Katambi amesisitiza kuwa hakuna sababu ya kuwepo kwa ucheleweshaji katika usajili wa biashara au kuwa kikwazo katika urasimishaji wa biashara. Badala yake, BRELA inapaswa kuwa daraja na si ukuta katika usajili wa biashara na kampuni ili kuendana na kasi ya maendeleo.
Kwa upande wake, Bi Loy Mhando Mkurugenzi wa Miliki Ubunifu akimuwakilisha Bw Godfrey Nyaisa, Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, amesema kuwa maelekezo yaliyotolewa na Naibu Waziri yanawakumbusha kuwa huduma zinazotolewa zinalenga kuwahudumia wananchi wa Tanzania.
Ameongeza kuwa ni wajibu wa BRELA kuendelea kuboresha mifumo yake ili kuhakikisha Watanzania wanapata huduma kwa haraka na kwa ufanisi.





