_Ataka maeneo yaliyokithiri kwa rushwa yapewe kipaumbele_
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema ni lazima yafanyike mapitio ya haraka kwenye tamko la mali na madeni na yawe na madaraja kwa sababu kuna maeneo ambayo bado rushwa imekithiri lakini watumishi wake hawajajumuishwa kwenye mfumo kama viongozi wa umma.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Alhamisi, Desemba 11, 2025), alipozungumza na Viongozi na Watendaji wa Ofisi ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, alipotembelea ofisi hizo zilizopo Mtaa wa Tambuka Reli, Jijini Dodoma.
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuiagiza Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kuhakikisha uadilifu unasimamiwa kuanzia katika sheria, kanuni na utekelezaji ili rasilimali za Taifa ziweze kuwanufaisha wananchi wote.
Amesema kuwa yapo maeneo ambayo fedha za umma huwa zinapotea hivyo yawekewe uangalizi wa kutosha. “Bado kuna kazi kubwa katika usimamizi wa maadili ya umma, suala hili Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amelisisitizia sana”
Ameiagiza taasisi hiyo ishirikiane na taasisi nyingine ikiwemo ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ili kuhakikisha wanaziba mianya yote ya rushwa kwa kuchunguza matamko yanayowasilishwa na viongozi kama yamejazwa kwa usahihi.
“…Bainisheni maeneo yenye rekodi za rushwa na yapewe kipaumbele; fomu zijazwe kuendana na uhalisia wa taarifa za mhusika. Lazima kila mtu aogope mali ya umma, msipochunguza, wananchi watachunguza wenyewe.”
Mheshimiwa Waziri Mkuu ametolea mfano maeneo ambayo yanatuhumiwa kuwa na mianya ya rushwa ni pamoja na michakato ya manunuzi, utiaji saini wa mikataba mbalimbali na maeneo ya makusanyo.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete amesema kuwa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ina kazi kubwa ya kuhakikisha nchi inaendeshwa kimaadili.







