
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imepokea magari mawili aina ya Land Cruiser Prado kutoka Taifa la Qatar kwa ajili ya kuhudumia viongozi wanaokuja kwa ziara za kitaifa na kikazi nchini.
Qatar kama mshirika wa maendeleo ya uchumi wa Tanzania alikubali ombi na ametoa magari hayo mapya kufuatia ombi la magari na pikikipiki za kuhudumia viongozi wa nje wawapo katika ziara nchini huku wakiendelea na mchakato wa kuleta pikipiki sita.
Akizungumza katika ofisi ndogo za wizara jijini Dar es Salaam baada ya kukabidhiwa nyaraka za magari hayo, Mheshimiwa Waziri, Balozi mahmoud Thabit Kombo (Mb.) ameishukuru Qatar kwa kuwa mdau mkubwa wa maendeleo Tanzania na kuahidi kutumia vyema misaada hii ili kuweza kutatua changamoto zinazojitokeza katika kazi.
Akimkabidhi funguo za magari hayo Afisa Usafirishaji Mkuu, Bw. Maulid Mkenda, Mhe. Waziri Kombo amemhimiza kuyatunza magari hayo ili yadumu na kuleta tija na ufanisi.
Qatar pia imekuwa ikitoa ushirikiano katika masuala ya ajira kwa vijana kwa kutoa nafasi za ajira kwa madereva wa Kitanzania nchini Qatar huku nafasi nyingine zikiendelea kuja na kutangazwa.





