
Na Mwandishi Wetu, WMTH — Dar es Salaam
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb), ameuelekeza uongozi wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) kuongeza uwekezaji katika maeneo ya kimkakati, yakiwemo mradi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, huduma ya Fibre to Home, pamoja na huduma za kuhifadhi data, ili kuongeza ushindani na kulikuzia shirika hilo uwezo wa kibiashara.
Aidha, ameagiza pia kuimarishwa kwa huduma za mawasiliano nchini wakati wa ziara yake ya kikazi katika Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) leo, Novemba 26, 2025, jijini Dar es Salaam. Ziara iliyolenga kufanya mapitio ya utendaji wa shirika na kujadili mikakati ya kulifanya liendane na mahitaji ya sasa ya Uchumi wa kidijitali.

Akiambatana na Naibu Waziri, Mhe. Dkt. Switbert Zacharia Mkama (Mb), Naibu Katibu Mkuu, Bw. Nicolaus Merinyo Mkapa, pamoja na menejimenti ya wizara, Mhe. Kairuki alipokea taarifa ya utendaji iliyowasilishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa TTCL, CPA Moremi Marwa.
Katika ziara hiyo, Waziri alitembelea Network Operation Center (NOC) na National Internet Data Centre, vitengo vinavyosimamiwa na TTCL kwa ajili ya kudhibiti na kufuatilia huduma za mtandao pamoja na miundombinu muhimu ya mawasiliano ya taifa.
Akizungumza baada ya kukamilika kwa ziara, Mhe. Kairuki aliwapongeza watumishi wa TTCL kwa hatua kubwa za maendeleo zilizofikiwa, huku akisisitiza haja ya kuongeza kasi ya uboreshaji wa huduma ili kuhakikisha wananchi mijini na vijijini wanapata mawasiliano ya uhakika. Pia alisisitiza umuhimu wa kuongeza watumishi, kuwajengea uwezo, kuboresha miundombinu, na kuwekeza katika huduma za data zinazochochea uchumi wa kidijitali.
Kwa upande wake, Naibu Waziri, Mhe. Dkt. Switbert Zacharia Mkama (Mb), aliitaka TTCL kuimarisha ubora wa huduma zinazotolewa kupitia minara ili kupunguza changamoto za mtandao hafifu, hususan vijijini. Pia alihimiza utafutaji wa masoko mapya ya Mkongo wa Taifa pamoja na kuendeleza ubunifu utakaoisaidia TTCL kubaki katika ushindani wa soko.
Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa TTCL, CPA Moremi Marwa, alimshukuru Mhe. Waziri kwa ziara hiyo na maelekezo aliyoyatoa, akiahidi kuwa shirika litaendelea kuongeza ubunifu, kuboresha huduma kwa wananchi na kusimamia kikamilifu miundombinu ya taifa. Alibainisha kuwa TTCL ina dhamira ya kuwa taasisi ya kisasa inayokwenda sambamba na mahitaji ya maendeleo ya kidijitali kwa manufaa ya watanzania.
http://TTCL KUONGEZA UWEKEZAJI WA KIMKAKATI KUIMARISHA BIASHARA NA HUDUMA :WAZIRI KAIRUKI.




