Home BUSINESS ZITTO KUJA NA MPANGO WA BOTI ZA UMEME KWA WAVUVI, KIGOMA

ZITTO KUJA NA MPANGO WA BOTI ZA UMEME KWA WAVUVI, KIGOMA

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

Mgombea ubunge jimbo la Kigoma mjini kupitia ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amewaahidi wavuvi katika jimbo hilo kuwa atakaposhinda nafasi ya ubunge na chama chake kupata madiwani, atakuja na mkakati utakaowawezesha wavuvi kutumia boti za umeme ili kupunguza gharama za uzalishaji.

Hatua hiyo inatokana na wavuvi wanaofanya shughuli zao katika ziwa Tanganyika lililopo jimboni hapo mkoani Kigoma, kutumia gharama ya zaidi ya shilingi 300,000 kwenye mafuta wanapokwenda kuvua samaki na kurudi nchi kavu.

Kauli hiyo imetolewa jana, Oktoba 19, 2025 na Zitto, wakati wa mkutano wa kampeni uliofanyika katika kata ya Kibirizi alipokuwa akimnadi mgombea udiwani wa chama hicho katika kata hiyo, Yunus Ruhomvya.

Zitto amesema akichaguliwa kuwa mbunge, atafanya ziara katika nchi za China na Japan kutembelea makampuni yanayozalisha mashine za umeme za boti, ambapo kupitia mpango atakaokuwa ameuandaa watafanya majaribio ili kujua ni mashine gani za umeme zitatumika kwenye boti za wavuvi wa ziwa Tanganyika.

“Nataka twende tukafanye kazi ya kuona namna gani tutaweza kitumia mashine za boti za umeme badala ya mafuta ili kupunguza gharama, hivi sasa kuna bodaboda na magari ya umeme inawezekana kabisa kuwa na boti za umeme”, alisema Zitto

Aidha, aliahidi kupambana kupunguza utitiri wa tozo katika sekta ya uvuvi jimboni hapo kwa kuhakikisha wavuvi wanakuwa na vitambulisho maalum badala ya kuwa na leseni lukuki wanapohitaji kufanya shughuli zao.

“Tunataka mvuvi awe na kitambulisho ambacho kitamtambua kama mvuvi na sio leseni za kukata kila mwaka, kama tingo au kondakta hana leseni mvuvi nae hatakuwa na leseni nipeni kazi nikapambanie mambo haya”, aliongeza Zitto

Zitto anaamini mazingira wezeshi katika seta ya uvuvi yatakwenda kuwanufaisha wananchi wa jimbo lake kutokana na sekta hiyo kuwa shughuli kuu ya uchumi katika manispaa ya Kigoma ujiji, ambapo asilimia 30 ya kipato cha manispaa hiyo kinatokana na uvuvi.