Home LOCAL DKT.SAMIA AHIDI KUONGEZA AJIRA KWA VIJANA.

DKT.SAMIA AHIDI KUONGEZA AJIRA KWA VIJANA.

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa awamu ya sita na Mgombea wa nafasi hiyo katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi CCM ameeleza mara zote tangu kuanza kwa kampeni zake kuwa anatambua nyenzo kubwa ya kuwawezesha wananchi kuongeza kipato na kuondokana na umaskini ni kuongeza fursa za ajira kwa kuongeza shughuli za kiuchumi kwenye Jamii.

Ameahidi kuweka mazingira sahihi ya kuzalisha fursa za ajira kwa Vijana na kuwawezesha wananchi kiuchumi hususan makundi maalumu ya Vijana, wanawake, watu wenye ulemavu pamoja na Wazee akisema lengo la CCM katika Miaka mitano ijayo ni kuzalisha ajira zenye tija zisizopungua Milioni nane katika sekta rasmi na isiyo rasmi, mpango ukiwa nusu ya ajira hizo zizalishwe kwenye sekta rasmi.

Dkt. Samia ameahidi kuwa kwa kutambua nafasi ya uzalishaji Viwandani katika kuchochea na kukuza fursa za ajira, kwa kipindi kijacho wataanzisha na kutekeleza programu maalumu ya ujenzi wa miundombinu ya Kongani za viwanda vidogo na vya Kati kwa kila mkoa na Wilaya, lengo likiwa ni kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, uvuvi, ufugaji, misitu na madini huku pia akiahidi kuendelea kuweka mazingira rafiki ya kikodi kwaajili ya Kongani hizo za viwanda.

Ilani anayoinadi Dkt. Samia imeahidi pia kuanzisha dirisha maalumu kwaajili ya mitaji ya kuanzisha kampuni changa, kuanzisha maeneo maalum ya uendelezaji wa bunifu na teknolojia zinazoibuliwa ili kuzalisha ajira kwa Vijana, kuweka mazingira wezeshi kuchochea uanzishwaji na usajilu wa makampunu ya kibiashara kama sehemu ya kurasimisha sekta isiyo rasmi pamoja na kuanzisha vituo maalum vya mafunzo stadi kwaajili ya kuandaa Vijana kushindana kupata fursa za ajira nje ya nchi (skills development Centre for Overseas Employment).

Aidha tutapitia upya mifuko ya uwezeshaji wananchi kiuchumi ili kuwa na mfumo mmoja na imara na wenye uwezo wa kuhudumia makundi mbalimbali ya wananchi pamoja na kuanzisha programu naalumu ya hamasa na mafunzo ili kuweza kutumia fursa za ajira nje ya nchi.” Amesema Dkt. Samia akinukuu Ilani ya 2025/30.

Ahadi nyingine katika sekta ya uwezeshaji wananchi kiuchumu ni pamoja na kuweka mazingira wezeshi ya kisera na Kimkakati kwa kuhamasisha uanzishwaji na kuimarisha makampuni ya Vijana na Vyama vya ushirika vyenye kujiendeleza kibiashara kwenye Halmashauri zote nchini ili yaweze kupata mikopo, mitaji na nyenzo kwa lengo la kuwawezesha wananchi wengi zaidi wakiwemo wahitimu wa elimu ya juu kujiajiri na kutoa ajira kwa wengine.