
▪Aipongeza STAMICO kwa kusambaza Nishati safi ya kupikia nchi nzima, kwa kasi.
▪Azitaka Taasisi nyingine kuiga mfano wa Magereza
▪Ashuhudia vibe la mawakala wa STAMICO – Wanawake na Samia, awapongeza
▪MD STAMICO almaarufu “Mjomba” naye awaahidi makubwa zaidi Wanawake na Samia
Moshi. 30/8/2025
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa amewataka Wananchi kuanza kutumia Nishati safi na salama za kupikia ili kujiepusha na madhara yanayotokana na utumiaji wa Nishati zisizo salama na zinazoongeza hewa ya ukaa.
Akizungumza katika hafla ya Uzinduzi wa Nishati safi ya kupikia Magerezani, iliofanyika katika viwanja vya ndani ya gereza la Karanga, Manispaa ya Moshi, Mheshimiwa Waziri Mkuu aliwahimiza Wananchi kuanza kutumia Nishati safi ili kulinda afya zao na Mazingira.
“Matumizi ya nishati za kuni na mikaa hayaleti tu tishio kwa afya zetu kupitia moshi na kemikali hatarishi, bali pia husababisha ukataji miti kwa kiwango kikubwa. Kwa kutumia nishati safi za upishi, tunalinda misitu yetu pamoja na afya ya umma,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.
Waziri Mkuu Majaliwa alizihimiza pia Taasisi zote zinazohudumia watu zaidi ya mia moja kuanza kutumia Nishati safi ya kupikia mara moja.
Kwa upande mwingine, Waziri Mkuu aliipongeza STAMICO kwa kuendelea kuwa Taasisi ya mfano katika kutekeleza ajenda ya Nishati Safi kwa vitendo. Alitoa pongezi kwa STAMICO kwa kuweza kuisambaza Nishati safi ya kupikia kwa kasi zaidi.
Naye, Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza (CGP) Jeremiah Katungu amesema kuwa utumiaji wa Nishati safi ya kupikia Magerezani umeongeza usalama wa wafungwa ambao sasa hawahitaji kwenda kutafuta kuni kwenye mapori.
“Matumizi ya Nishati safi yamekuwa mkombozi kwa wafungwa na hata wale wanaowaandalia wafungwa Chakula, kwa hili tumepiga hatua moja kubwa sana” alisisitiza CGP Jeremiah Katungu
Wakati akijibu maswali ya Waziri Mkuu, Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dkt. Venance Mwasse aliielezea Nishati safi ya kupikia ya Rafiki Briquettes, kuwa ni salama kwa matumizi ya Kupikia na imepitia mchakato wa Kiwandani wa kupunguza hewa ukaa na pia ukali wa kuwaka.
Aliendelea kufafanua kwamba Nishati hii imepitia viwango vyote vya ubora na usalama ikiwemo kuthibitishwa (kuwa bora) na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).
“STAMICO imejipanga kuendelea kuisambaza Nishati hii kwa kasi zaidi kupitia mawakala wake ambao ni Taasisi ya *Wanawake na Samia* nchi nzima. tumeshaanza mchakato wa kununua Pikipiki za kubebea mizigo ili kuongeza wepesi wa kuisambaza Nishati ya Rafiki Briquettes kwenye maeneo yote nchini, hasa vijijini” aliongezea Dkt. Mwasse




