Home LOCAL KURA ZOTE BUTINZYA TUMPIGIE DKT. SAMIA – DKT. BITEKO

KURA ZOTE BUTINZYA TUMPIGIE DKT. SAMIA – DKT. BITEKO

Mgombea Ubunge wa Jimbo la Bukombe kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Ndugu Doto Mashaka Biteko amewahimiza wananchi wa Kata ya Butinzya, Wilayani Bukombe kumpigia kura mgombea wa Urais kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM)Dkt. Samia Suluhu Hassan ili aendelee kuongoza na kusimamia miradi ya maendele iliyokwishaanzishwa na hivyo kuwaletea maendeleo.

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

Dkt. Biteko amesema hayo Septemba 30, 2025 wakati wa mkutano wa kampeni katika Kata ya Butinzya wilayani Bukombe mkoani Geita ikiwa ni sehemu Kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu.

Amesema wananchi wanalo jukumu la kujotokeza kwa wingi kupiga kura na watakapopiga kura maana yake ni kutimiza wajibu wao kidemokrasia ambao utawawezesha kutimiziwa mahitaji yao kwa kujengewa miradi ya maji, umeme, barabara, hospitali na shule.

Amesema katika miaka mitano iliyopita wananchi hao wakishiriki katika kutekeleza miradi ya maendeleo iliyolenga kutatua changamoto za Bukombe na sasa jukumu lililopo mbele ni kuboresha na kuongeza miundombinu kwa maslahi mapana ya wananchi wa Wilaya
ya Bukombe na Taifa kwa ujumla.

“Kipindi kilichopita hapakuwa na barabara lakini leo tumeifungua miundombinu ya barabara kutoka Butinzya hadi Isemabuma na maeneo mengine. Changamoto ya maji tunaifanyia kazi na tutahakikisha yatapatikana katika umbali usiozidi mita 400, tunajenga zahanati nyingine na tunataka kuongeza madarasa na kukarabati shule,” amesema Dkt. Biteko.

Ameongeza maendeleo yaliyopatikana ni uwezeshaji kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan “ Haya yote anayoweza kuyafanya ni Dkt. Samia, mimi siwezi kufanya haya yote bila msaada na uwezeshaji wake. Hivyo, niwaombe wananchi wote 7,111 mliojiandikisha mjitokeze na kumpigia kura Dkt. Samia,”

Akiendelea na kampeni zake katika Kata ya Igulwa, Dkt. Biteko amesema kuwa Rais Samia amedhamiria kuleta maendeleo katika Wilaya ya Bukombe kwa kuendelea kujenga barabara za lami ambapo barabara ya Ushirombo kwenda Katoro imeanza kujengwa.

Pia, amesema Rais Samia ametoa kibali kwa ajili ya kuchimba madini katika Pori la Kigosi ili kuwasaidia wananchi hapo kujipatia kipato.

Dkt. Biteko amebainisha kuwa katika Shule ya Sekondari Bukombe kupitia ufadhili wa Ubalozi wa India wanajenga kituo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ili wanafunzi wa Bukombe waweze kuwa na elimu ya masuala ya teknolojia kwa manufaa yao.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Umoja wa Vijana Taifa wa Chama Cha Mapinduzi Tanzania Bara na Mjumbe wa Halmashauri Kuu, Mussa Mwakitinya amesema Ilani ya CCM inaweka wazi malengo ya Serikali kukuza uchumi wa Mtanzania na kuongeza ustawi wa jamii.

“ Ilani yetu imeeleza hapa kuwa Dkt. Samia ana mpango wa kumuona kila Mtanzania ana maisha mazuri, anatenga bilioni 99 kwa ajili ya wanawake na shilingi bilioni 96 kwa ajili ya vijana. Hapa Bukombe CCM italeta shilingi bilioni 2 kwa ajili ya mikopo,” amesema Mwakitinya.

Naye, Mgombea wa Udiwani Kata ya Butinzya, Kwizi Mathias amewaeleza wananchi hao kuwa endapo watawachagua wagombea wa CCM Oktoba 29 watahakikisha wanafanyia kazi changamoto chache zilizopo katika Kata hiyo ikiwemo upatikanaji wa maji.

Kwa upande wake, Mgombea Udiwani wa Kata ya Igulwa, Richard Mabenga amewaomba wananchi hao kuendelea kumuamini na kumchagua tena katika nafasi ya udiwani.

Aidha, amesema waichague CCM kwa kuwa pamoja na miradi mingine wamejenga shule ya sekondari ya Dkt. Biteko, sekondari ya amali ya Igulwa iliyogharimu shilingi milioni 580.

Sambamba na hayo wameanza kujenga mtandao wa barabara za lami , wamechimba kisima, wamejenga Chuo Kikuu hivyo Oktoba 29 wananchi wawachague wagombea wa CCM.