
– Ni kuhusu ujenzi nyymba za, majengo ya biashara
-Kujielekeza kweye miradi inayojibu changamoto ya nyumba bora
-Yaongeza nguvu miradi ya kimkakati
Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.


Katika juhudi za kuimarisha ustawi wa jamii, miundombinu na uchumi jumuishi, Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limeendelea kuwa kinara wa utekelezaji wa ajenda ya Taifa ya makazi bora.
Kupitia miradi ya kimkakati inayotekelezwa kote nchini, NHC si tu linajenga nyumba, bali linajenga matumaini mapya kwa maelfu ya Watanzania.
Mwaka 2025 umeshuhudia mwelekeo mpya wa NHC, likiongozwa na Dira ya Taifa na mahitaji ya jamii. Katika ziara ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Deogratius Ndejembi, Makao Makuu ya NHC, alielezwa kuhusu mafanikio makubwa ya shirika hilo kupitia taarifa ya Mkurugenzi wa Ujenzi, Mhandisi Godwin Maro.
Katika Jiji la Dodoma, NHC linaendeleza Mradi wa Samia Iyumbu Apartments, unaolenga kujenga zaidi ya nyumba 300 kwa wananchi wa kipato cha kati na cha juu. Mradi huu umezingatia mahitaji ya kisasa ya familia, ikiwemo shule, barabara na huduma za afya.


Jijini Dar es Salaam, NHC linaendelea na ujenzi wa Mtanda Commercial Complex ambao umefikia asilimia 75 ya utekelezaji. Mradi huo wa thamani ya Shilingi bilioni 4.2 unalenga kuwa kitovu cha biashara, ofisi, maduka na huduma nyingine za kijamii. Pia katika eneo la Temeke, linaendelea na ujenzi wa zaidi ya nyumba 300 chini ya Samia Kijichi Housing Scheme, kwa ajili ya watu wa kipato cha kati.

Katika Jiji la Tanga, NHC limeanza ujenzi wa mradi wa Mkwakwani, wenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 7, ukilenga kuchochea uwekezaji katika ukanda wa kaskazini na kutoa ajira kwa vijana. Katika mji wa Singida, kazi ya ujenzi wa mradi wa 2F imefikia hatua ya kuweka slab, ikiwa ni fursa kwa mafundi na watoa huduma wa ndani.
Sekta ya madini haijaachwa nyuma, ambapo NHC linaendelea na ujenzi wa Soko la Madini la Mirerani, kwa lengo la kuongeza usalama wa biashara na thamani ya madini, hasa Tanzanite. Mradi huu ni sehemu ya mkakati wa kuwawezesha wachimbaji wadogo kunufaika zaidi na rasilimali za Taifa.

Jijini Morogoro, Mradi wa 2H Plaza wenye thamani ya Shilingi bilioni 2.6 umeanza kuaminika sokoni, ambapo baadhi ya nyumba zimeuzwa kabla ya kukamilika kwa ujenzi. Hii inaonyesha kuaminika kwa NHC kama mtoa huduma bora wa makazi.
Mkoani Kagera, mradi wa Kashozi unaendelea kwa hatua ya awali ya ujenzi, ukiwa na thamani ya Shilingi bilioni 1.8. Huu ni mfano wa usambazaji wa miradi hadi pembezoni mwa nchi. Katika eneo la Njendengwa jijini Dodoma, maandalizi ya mradi wa nyumba zaidi ya 120 yanaendelea, kama jibu kwa ongezeko la watumishi na ukuaji wa mji.


Katika Mkoa wa Tabora, NHC linaendelea na Tabora Commercial Complex, mradi wa kisasa utakaowezesha wakazi kupata huduma karibu na makazi yao. Arusha, Mradi wa Meru Shops umeongezwa kutoka ghorofa moja hadi mbili, ukilenga wafanyabiashara wa kati na wadogo.
NHC pia inaendeleza ukarabati wa majengo ya zamani, kuboresha miundombinu, mifumo ya maji, umeme na mandhari kwa kutumia teknolojia mpya. Hii ni juhudi ya kulinda historia huku yakirejeshwa katika viwango vya sasa.


Katika eneo la Kawe jijini Dar es Salaam, Samia Housing Scheme unaendelea na tayari nyumba 560 zimekamilika, huku nyingine 560 zikitarajiwa kuanza kujengwa hivi karibuni. Mradi huu ni wa mfano kwa kutoa makazi bora kwa gharama nafuu.
Zaidi ya hayo, NHC linaendelea na ujenzi wa maghala matatu ya kisasa kwa ajili ya kuhifadhi bidhaa, ili kuongeza mapato ya ndani na kusaidia shughuli za kibiashara na usafirishaji.

Kupitia miradi hii, NHC limejidhihirisha kuwa taasisi ya umma inayoweza kutekeleza miradi mikubwa kwa ubora, kujitegemea kifedha, na kuchangia ajenda ya maendeleo ya Taifa kwa vitendo. Shirika hili halijengi tu nyumba, bali linajenga heshima, utu na ustawi wa jamii.
Kwa kasi ya utekelezaji inayoonekana sasa, NHC linazidi kuthibitisha kuwa mshirika wa kweli wa maendeleo ya Taifa, likiwasha taa ya matumaini kwa Watanzania wengi wanaotamani maisha bora kupitia makazi bora.





