http://RAIS WA JAMHURI YA MSUMBIJI MHE CHAPO KUANZA ZIARA YA SIKU TATU TANZANIA
Rais wa Jamhuri ya Msumbiji, Mhe. Daniel Francisco Chapo anatarajia kuanza Ziara ya Kiserikali ya siku tatu hapa nchini kuanzia leo tarehe 07 Mei, 2025, kufuatia mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Hii ni Ziara ya kwanza ya Kiserikali ya Mhe. Rais Daniel Chapo kuifanya nchini Tanzania tangu aapishwe kuwa Rais wa Jamhuri ya Msumbiji tarehe 15 Januari, 2025.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Raia Ikulu Sharifa Nyanga imesema Tanzania na Msumbiji zina uhusiano wa kihistoria na kidugu ulioasisiwa na Waasisi wa nchi hizi mbili wakati wa ukombozi wa nchi za Kusini mwa Bara la Afrika, Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Rais wa kwanza wa FRELIMO Hayati Eduardo Chivambo Mondlane na Rais wa kwanza wa nchi hiyo Hayati Samora Moisés Machel.
Aidha, Ziara hii itadumisha mahusiano yaliyopo, kuimarisha ushirikiano kwenye sekta mbalimbali pamoja na kufungua fursa mpya za ushirikiano zenye maslahi kwa pande zote mbili.
Rais Samia atampokea mgeni wake kesho tarehe 08 Mei, 2025 Ikulu jijini Dar es Salaam na kufanya mazungumzo rasmi pamoja na kushuhudia uwekaji saini Mikataba na Hati za Makubaliano (MOU) katika sekta mbalimbali kwa ajili ya kuimarisha ushirikiano.
Vile vile, Rais Chapo atapata fursa ya kutembelea sehemu mbalimbali ikiwemo Hospitali ya Taifa Muhimbili, Kituo cha Urithi wa Ukombozi wa Afrika na mradi wa kimkakati wa Reli ya Kisasa (SGR) ili kujifunza na kuangalia fursa za ushirikiano. Pia katika ziara hiyo nchini, Rais Chapo atapata fursa ya kutembelea Zanzibar ambapo atafanya mazungumzo na mwenyeji wake Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt Hussein Ali Mwinyi na kutembelea miradi mbalimbali ikiwemo Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu na Soko la Samaki la Malindi.
Rais Chapo atahitimisha ziara yake nchini tarehe 09 Mei, 2025 na kuagwa rasmi na Rais Dkt.
Samia Ikulu jijini Dar es Salaam.