Serikali ya kijeshi ya Burkina Faso imesema siku ya Jumatatu imefanikiwa kuzuia “njama kubwa” iliyokuwa ikipangwa kwa lengo la “kuleta machafuko makubwa”, ikisema kwamba inaamini wapangaji wa njama hiyo wako katika nchi jirani ya Ivory Coast.
Tangu Septemba 2022, Burkina Faso inatawaliwa na jeshi kufuatia mapinduzi yaliyoongozwa na Kapteni Ibrahim Traoré, ambaye mara kadhaa ameishutumu Ivory Coast kwa kuwahifadhi wapinzani wake.
Ingawa Traoré ameahidi kurejesha usalama nchini humo, utawala wake umekuwa ukikandamiza wanaopinga serikali na kuhusishwa na matukio ya utekaji nyara na kukamatwa kiholela kwa raia wanaoonekana kuwa wapinzani wa utawala huo wa kijeshi.
Waziri wa Usalama, Mahamadou Sana, alisema kupitia taarifa iliyosomwa kwenye runinga ya taifa:
“Uchunguzi makini wa idara ya ujasusi umebaini njama kubwa iliyokuwa ikipangwa dhidi ya nchi yetu, ambayo lengo lake kuu lilikuwa ni kueneza machafuko makubwa.”
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, njama hiyo ilipangwa kufikia kilele chake Jumatano, Aprili 16, 2025, kwa shambulio dhidi ya ikulu ya rais likiongozwa na kundi la wanajeshi waliovutwa kwenye mpango huo na “maadui wa taifa”.
Waziri huyo alidai kwamba “vichwa vya mpango huo” wapo Ivory Coast, akiwataja maafisa wa zamani wa jeshi – Meja Joanny Compaoré na Luteni Abdramane Barry.
Taarifa kutoka vyanzo vya usalama zilieleza kuwa wanajeshi kadhaa – wakiwemo maafisa wawili – walikamatwa wiki iliyopita kwa tuhuma za kupanga njama ya “kuipindua serikali”.
Mwaka jana, Kapteni Traoré pia aliituhumu Ivory Coast kuwa ni “kitovu cha operesheni za kuiyumbisha Burkina Faso”.