
Akizungumza na Wanahabari Leo,Machi 05, 2025, jijini Dar es Salaam, Afisa Mtendaji Mkuu Bw. Godfrey Nyaisa amesema BRELA ni Msajili wa Makampuni kwa mamlaka iliyopewa chini ya Kifungu cha 400A cha Sheria ya Kampuni Sura 212, imefuta kampuni kwa sababu za kampuni hizo zimekukiuka masharti ya Kifungu cha 400A (1) (e) cha Sheria tajwa hapo juu, kwa kufanya shughuli za kibiashara nje ya madhumuni yaliyoainishwa katika Katiba za kampuni hizo na Miongozo ya Uendeshaji wa Kampuni wakati wa usajili.
Amesema kifungu hiki kikikiukwa, sheria inamtaka Msajili kuchukua hatua chini ya Kifungu hicho 400A (1) (e) ambazo ni kuijulisha kampuni kuhusu ukiukwaji na hatua anazokusudia kuzichukua kwa kampuni husika. Sheria inaendelea kueleza kuwa, endapo kampuni itashindwa kutoa maelezo, au kutoa maelezo yasiyoridhisha, Msajili atafuta kampuni husika kwenye Rejista ya Kampuni.
Hivyo, kwa mujibu wa Kifungu cha 400A (1) (e) Msajili amezijulisha kampuni husika kuhusu kusudio la kuzifuta kupitia notisi zilizotolewa kati ya tarehe 2 na tarehe 26 Januari, 2025, na kwa kuwa kampuni hizo hazikuwasilisha maelezo yoyote kama zilivyotakiwa chini ya kifungu 400A (2), Msajili amezifuta rasmi kampuni hizo ambazo zipo kwenye Rejista ya Kampuni kuanzia tarehe 27 Februari, 2025 ambazo ni, LBL Mtwara Media Company Limited (Na. 181289972), LBL Morogoro Media Company Limited (Na. 179770873), LBL Geita Advertising Media Limited (Na. 180439242), LBL Mbeya Media Limited (Na. 179978326) LBL Future Vision Advertising Agency Company Limited (Na. 181302259). 6. LBL Mbezi Advertising Media Company Limited (Na. 180582835), LBL Ubungo Media Limited (Na. 180960333) LBL Mabibo Media Company Limited (Na. 181117346), LBL Mbagala Media Company Limited (Na. 181248874) LBL Gongo la Mboto Media Advertising Company Limited (Na. 181513438), na LBL Dar es Salaam Kigamboni Advertising Company Limited (Na. 180046992).

