Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewahakikishia Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuwa Tanzania itaendelea kutoa ushirikiano katika kushughulikia mgogoro unaoendelea Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo (DRC).
Aidha, Rais Dkt. Samia ametoa rai kwa Jumuiya hizo mbili kuchukua hatua kuhakikisha kuwa DRC, ambayo ni mwanachama wa EAC na SADC, inakuwa salama na mgogoro unaoendelea nchini humo unamalizika.
Rais Dkt. Samia ameyasema hayo leo wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa pamoja wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa EAC na SADC uliofanyika katika Ikulu ya Dar es Salaam ili kujadili hali ya usalama Mashariki mwa DRC.
Rais Dkt. Samia ameeleza kuwa hali inayoshuhudiwa Mashariki mwa DRC haikubaliki na ipo haja ya kuchukua hatua za haraka kumaliza mgogoro huo unaoleta mateso kwa wananchi. Rais Samia amesema ana imani kuwa Mkutano huo utatoka na maazimio ambayo yatawezesha wananchi wa Mashariki mwa DRC kuishi amani.
Kwa upande wake Rais wa Jamhuri ya Kenya, ambaye pia ni Mwenyekiti wa EAC, Mhe. Dkt. William Samoei Ruto amesema mgogoro unaoendelea Mashariki mwa DRC hautamalizwa kwa kutumia silaha bali kwa njia za kidiplomasia kupitia mazungumzo, kusikilizana na kushauriana. Aidha, amewataka wadau wote kushirikiana na EAC na SADC ili kumaliza mgogoro huo ambao unaendelea kugharimu maisha ya wananchi wasio na hatia.
Kwa upande wake Rais wa Jamhuri ya Zimbabwe na Mwenyekiti wa SADC, Mhe. Dkt Emmerson Dambudzo Mnangagwa amesema hali inayoendelea Mashariki mwa DRC inaathiri bara zima la Afrika, hivyo nchi za Afrika zinapaswa kushikamana kama zilivyoshikamana wakati wa kupigania uhuru wa bara la Afrika.
Sharifa B. Nyanga
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu