Home LOCAL NIRC YASHUSHA NEEMA PWANI

NIRC YASHUSHA NEEMA PWANI

KUJENGA VISIMA VYA UMWAGILIAJI VITANO

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

NIRC Pwani

Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC), imesaini mkataba wa mradi wa uchimbaji visima vitano vya umwagiliaji katika Mkoa wa Pwani.

Visima hivyo ni sehemu ya Mpango wa Serikali wa Programu ya Mfumo Himilivu ya Chakula kwa Kuzingatia Matokeo ili kuhakikisha nchi inakuwa na chakula cha kutosha.

Visima hivyo vinatarajiwa kutumika katika kilimo cha mbogamboga
vitachimbwa katika wilaya tano za mkoa huo.

Makubaliano hayo yametiwa saini leo Jumanne, Februari 11, 2025 katika Kijiji cha Gwata wilayani Kibaha Mkoa wa Pwani na Meneja wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Mkoa wa Pwani (NIRC), Injinia Ramadhani Lusonge na mwakilishi wa Kampuni Paragon Engineering Ltd, Anold Kulanga itakayotekeleza mradi huo.

Akizungumza katika sherehe za utiaji saini mradi huo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Aboubakar Kunenge, Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Nickson Saimon amesema awamu ya kwanza itahusisha visima vinne vitakavyochimbwa katika Wilaya ya Kibaha, Kibiti, Chalinze na Rufiji.

Kwa mujibu wa Mkuu wa wilaya huyo, lengo la mradi huo ni kuhakikisha sekta ya kilimo cha Umwagiliaji inakua katika mkoa huo na kuchangia ukuaji wa uchumi na Pato la Taifa.

“Visima vitafungwa umeme wa Solar (jua) ili kuhakikisha umeme unakuwa wa uhakika wakati wowote hivyo kuwawezesha wakulima kulima mpaka misimu mitatu kwa mwaka badala ya mmoja kama ilivyozoeleka. “

” Lengo letu mkoa wa Pwani ni kufikisha visima 240 ifikapo mwaka 2030 kwani mpaka sasa tuna jumla ya visima 140 na kwa kasi hii ya Tume ya Umwagiliaji chini ya Rais Samia Suluhu Hassan tunaamini hilo tutatekeleza, ” alisisitiza Saimon.

Alisema katika awamu hii ya mradi huo itahusisha visima 35 katika wilaya saba za mkoa huo ambako kila wilaya itachimbiwa visima vitano.

Hata hivyo, Mkuu huyo wa Wilaya amewataka wananchi wanaonufaika na mradi huo kuhakikisha wanashirikiana kulinda miundombinu yake ili idumu na kuwanufaisha zaidi.

Awali Meneja wa NIRC Mkoa wa Pwani, Injinia Ramadhanj Lusonge alisema mradi huo ukikamilika utawanufaisha wananchi wa kijiji cha Gwata (Kibaha), Mwetemo (Chalinze), Mkupuka (Kibiti) na Mbwara (Rufiji).

Injinia Lusonge alisema zaidi ya Sh311 milioni zinatarajiwa kutimika kutekeleza mradi huo katika mikoa ya Pwani na Tanga.

Hivi karibuni Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) , Raymond Mndolwa alisema kwa mwaka huu wa fedha Tume inatarajia kuchimba visima 1,300 na kati ya hivyo visima 70 vitakahudumia mikoa 16 ikiwemo Pwani, Tanga, Mara, Songwe, Singida, Manyara, Dodoma, Lindi, Mtwara, Kigoma, Geita, Morogoro, Simiyu, Ruvuma na Njombe vitachimbwa na wakandarasi na visima vinavyobaki vitachimbwa kupitia mitambo inayonunuliwa.