Waziri wa Afya, Mhe. Jenista Mhagama leo amepokea msaada wa vifaa tiba mbalimbali vyenye thamani ya TZS. 125 Mil kutoka kwa Serikali ya Watu wa China ambavyo vitaisaidia Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kuboresha huduma za afya na kukabiliana na changamoto mbalimbali katika utoaji wa huduma za afya bora kwa wananchi.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano, Mhe. Mhagama amesema msaada huo ni sehemu ya kuadhimisha miaka 60 ya ushirikiano kati ya Tanzania na China katika sekta ya afya na kuongeza kuwa ushirikiano baina ya nchi hizo mbili utaendelea kuleta manufaa zaidi kwa pande zote ikiwemo kuendelea kuleta wataalam wa afya mabingwa wabobezi, vifaa vya kisasa vinavyotumia teknolojia ya hali ya juu ili kuongeza ubora wa huduma.
“Naupongeza uongozi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa kuwa na mchango mkubwa katika utekelezaji wa ushirikiano huu, msaada huu utachangia katika kuboresha utoaji wa huduma za afya na kutoa matokeo chanya kwa wananchi”, amesema Mhe. Mhagama
Kwa upande wake, Balozi wa China nchini Tanzania Mhe. Chen Mingjian ameishukuru Wizara ya Afya, Hospitali ya Taifa Muhimbili na timu ya madaktari kutoka China waliopo Tanzania kwa michango yao muhimu katika ushirikiano wa muda mrefu kati ya nchi hizi mbili katika sekta ya afya.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Mohamed Janabi, ameishukuru Serikali ya China kwa msaada huo na kuomba ushirikiano zaidi katika maendeleo ya rasilimali watu na utoaji wa teknolojia za kisasa.
“Ushirikiano huu ni fursa kwa madaktari wetu kupata mafunzo ya ubingwa nchini China ambayo yataboresha ujuzi wao na kuwafundisha teknolojia na mbinu za kisasa zinazohitajika katika huduma za afya,” amesisitiza Prof. Janabi.