_▪️Rais Dkt. Samia asema Jaji Werema alikuwa kiongozi mwenye misimamo_
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa leo Januari 02, 2025 amemwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuaga mwili wa marehemu Jaji Fredrick Werema ambaye aliwahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika kipindi cha kuanzia Mwaka 2009-2014.
Mheshimiwa Waziri Mkuu amesema kuwa Rais Dkt. Samia amesikitishwa na kifo cha Jaji Werema na amemtaja kama kiongozi shupavu aliyekuwa anazingatia maadili wakati wote na mwenye misimamo katika utendaji kazi wake. Tukio la kuaga Mwili wa Jaji Werema limefanyika katika Viwanja vya Karimjee Jijini Dar es Salaam.
“Mheshimiwa Rais anajua kwamba Marehemu amefanya kazi katika mihimili yote na anauzoefu mkubwa wa utendaji katika mihimili yote, mengi mazuri ameyatenda, Rais Dkt. Samia anawasihi wote muwe wavumilivu katika kipindi hiki kigumu na ametusihi tuendelee kumuombea na kuyaenzi yote aliyoyafanya katika utumishi wake”.
Kadhalika Mheshimiwa Majaliwa amewataka amewataka wanasheria na watanzania kwa ujumla kuyaenzi na kuyaendeleza yale yote mazuri aliyoyafanya jaji Werema enzi za uhai wake”
Kwa Upande wake Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa Jaji Werema alikuwa Mwanasheria mbobezi, mzalendo wa dhati na mara zote alitoa ushauri makini kwa maslahi ya Taifa, alikuwa mahiri ma mpenda haki. “Amefanya mengi mema kwa Taifa na ameacha alama ya kudumu nchini, Nilimteua kuwa Jaji kutokana na sifa zake katika utendaji”
Naye, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari amesema kuwa Marehemu Jaji Werema alikuwa ni mtu mwenye maono na mtaalam wa Sheria aliyejitolea na kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha sheria na haki zinatumika katika kuleta maendeleo kwa Taifa.
“Jaji Werema alifanya maboresho makubwa katika mfumo wa sheria na haki na alifanikiwa kwa kiasi kikubwa kuboresha na kuimarisha utawala wa sheria na kuwaendeleza, kuwafunda na kuwanyanyua wanasheria waliokuwa wanachipukia, alionesha uongozi wa aina yake katika nyakati ngumu pia aliweza kupigania maslahi ya Taifa”
Waziri Mkuu Mstaafu Jaji Joseph Warioba amesema kuwa Marehemu Jaji Werema atakumbukwa kwa mengi katika utumishi wake wa umma “Jaji Werema alikuwa mtu mwenye msimamo, akiamini kitu anafanya na kutenda vile vile, hakuwa na lugha za kuchanganya, alikuwa muadilifu na alilitumikia Taifa kwa uwezo wake wote”.
Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Ally Possi amesema kuwa Jaji Werema alikuwa mahiri na nguzo imara katika sekta ya sheria nchini kwani aliendelea kuhudumu katika sekta ya sheria hata baada ya kumaliza muda wake serikali. “Uimara wake katika maeneo mbalimbali ya sheria, uchapakazi wake umeacha alama katika sekta ya sheria nchini”.
http://WAZIRI MKUU AMWAKILISHA RAIS DKT. SAMIA KUAGA MWILI WA MAREHEMU JAJI WEREMA.