Home LOCAL WAZIRI BASHUNGWA AMETOA HOTUBA FUPI KUELEKEA SIKUKUU YA KRISMASI NA MWAKA MPYA.

WAZIRI BASHUNGWA AMETOA HOTUBA FUPI KUELEKEA SIKUKUU YA KRISMASI NA MWAKA MPYA.

http://WAZIRI BASHUNGWA AMETOA HOTUBA FUPI KUELEKEA SIKUKUU YA KRISMASI NA MWAKA MPYA.Nitumie nafasi hii kutoa wito kwa wasafiri na wasafirishaji, kuzingatia na kuheshimu
Sheria za Usalama Barabarani, ili kupunguza ajali zinazoepukika, ambazo mara nyingi zimekuwa zikisababisha vifo, majeruhi na hata kusababisha ulemavu kwa ndugu na wananchi wenzetu. Yapo matukio ya ajali ambayo yanatokana na uzembe wa madereva, ama wamiliki wa magari kutofanyia matengenezo ya mara kwa mara vyombo hivyo vya usafiri.

Kwa mfano, ajali iliyotokea tarehe 03 Disemba 2024 katika eneo la Kihanga,Wilaya ya Karagwe, Mkoani Kagera, watu 7 walifariki papo hapo na majeruhi 9.
Ajali nyingine iliyotokea jana usiku wa tarehe 18 Disemba, 2024 eneo la Mikese, Mkoa wa Morogoro, ambapo watu 15 walipoteza maisha na wengine 8 ni majeruhi.

Ndugu Waandishi wa Habari na Wananchi, Natoa wito kwa wasafirishaji na watumiaji wote wa vyombo vya moto, kufanya ukaguzi na matengenezo ya vyombo vya moto kila inapopaswa.

Na wale wenye tabia ya kuendesha vyombo vya moto ili mradi tu chombo kinawaka na kutembea; wenye tabia ya kwenda mwendokasi na kupuuza speed limit; wenye tabia ya kujaza abiria kupita kiasi; wenye tabia ya kunywa pombe na kuendesha vyombo vya moto; na tabia nyingine za aina hii zinazokiuka Sheria za
Usalama Barabarani kuacha tabia hizi mara moja kwani zinahatarisha maisha ya watanzania.

OLE WAKE ATAKAYEBAINIKA KUSABABISHA AJALI ZA KIZEMBE!
SERIKALI HAIKO TAYARI KUONA MAISHA YA WATANZANIA YANAWEKWA
REHANI, KWA UZEMBE WA WATU WACHACHE.

Hatuko tayari kuacha tabia za kizembe ziendelee kupoteza maisha ya watu, na wengine
kupata ulemavu, huku Sheria za kudhibiti uzembe zikiwa zipo. Tutachukua hatua kali kwa madereva na wasafarishaji wazembe. Ninaomba wasafiri mtupe ushirikiano, na kuunga mkono jitihada hizi, ili tuwe salama tunapokuwa barabarani.

Nitoe tahadhari kwa familia zinazotumia magari yao binafsi, kufanya matengenezo yamagari kabla ya safari, na kuacha utamaduni wa kuchukua mtu yeyote ambaye hana taaluma ya udereva, wala leseni, na hajapitia mafunzo ya kuendesha magari kwa kukwepa gharama. Kila familia ichukue tahadhari, hususani tunapoelekea mwisho wa mwaka.

Ulinzi wa Watoto Nyakati za Sikukuu Upo utamaduni mwingine kwenye sherehe za mwisho wa mwaka, wazazi kuwaacha watoto kwenda sehemu mbalimbali kwa ajili ya kusherehekea sikukuu, yakiwemo maeneo ya ufukweni au kwenye maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya michezo ya watoto, huku wakiwa peke yao. Niwaombe wazazi kuwalinda watoto na kutoruhusu watoto kwenda kutembea siku za sikukuu wakiwa peke yao.

Tumeshuhudia madhara mengi yakiwapata watoto hususani siku za sikukuu wanapokuwa peke yao. Shukrani kwa Amiri Jeshi Mkuu na Jeshi la Polisi; Ninampongeza IGP Camillus Wambura, Makamanda Wote, Maafisa na Askari wa Jeshi la Polisi, kwa kazi nzuri wanayofanya ya kuendelea kulinda amani ma utulivu ndani ya Nchi yetu, usalama wa raia na mali zao, kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama vilivyoko ndani ya Wizara na Nje ya Wizara yetu.

Ninamshukuru Mhe. Rais na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuliwezesha Jeshi la Polisi kupambana na uhalifu, na huku jitihada kubwa zikielekezwa katika kushirikiana na wananchi raia wema, katika kupata taarifa mapema ili kuzuia uhalifu kabla haujatokea.

Watanzania wenzangu tukumbuke, Kinga ni bora kuliko Tiba. Duniani kote Serikali za Nchi huru na za kidemokrasia, hutegemea Jeshi la Polisi katika Ulinzi na Usalama wa ndani ya Nchi. Kwa kiasi kikubwa Jeshi la Polisi linafanya kazi nzuri, na ndio maana tunalala na kuamka huku usalama wa raia na mali zikiwa salama na amani na utulivu vikiendelea kuwa Tunu yetu Kuu.

Taasisi yeyote ile haikosi changamoto, hata ndani ya Jeshi la Polisi tunakiri zipo
changamoto. Kwa niaba ya Serikali, naomba kuwaahidi wananchi kwamba tunaendelea kuzifanyia kazi changamoto hizi, usiku na mchana bila kuchoka.

Ndugu Waandishi wa Habari na Wananchi, Naomba nitumie nafasi hii kumuelekeza IGP Camillus Wambura kufanyia kazi masuala yafuatayo kuelekea sikukuu za Krismas na
Mwaka Mpya:
1) Kuimarisha ulinzi kwenye Nyumba za Ibada, na kufanya ukaguzi wa vyombo vya moto barabarani, pamoja na kuimarisha highway patrol usiku na mchana, kwa
mujibu wa Sheria, na bila kumwonea au kumpendelea mtu yeyote. Kila mmoja wetu akifuata Sheria za Usalama Barabarani na kufanya matumizi sahihi ya
barabara, tutasherehekea sikukuu hizi kwa usalama, amani na utulivu kwa kuwa
“Safari bila ajali inawezekana”.

2) Taarifa za ajali mbalimbali zimeonesha dosari kwa baadhi ya vizuizi na vituo vya
ukaguzi barabarani, kutozingatia matumizi sahihi ya barabara, na hivyo kusababisha ajali. Jeshi la Polisi lishirikiane na TANROADS) pamoja na TARURA, likague maeneo yote nchini yenye vizuizi ama vituo vya ukaguzi, kuangalia kama vimewekwa kwa kuzingatia Sheria, na tahadhari ya usalama kwa watumiaji wengine wa barabara.

Pale itakapokutwa vizuizi ama vituo vya ukaguzi vimewekwa bila kuzingatia
taaluma na uzingatiaji usalama wa watumiaji wengine wa barabara, wakutane na Taasisi au Mamlaka husika ili kuviondoa katika maeneo hatarishi, na kwa pamoja kukubaliana maeneo sahihi ya kuweka vituo hivyo.

3) Kumekuwa na matukio ya uhalifu yanayohusisha uhujumu wa miundombinu ya TANESCO, SGR, na miundombinu ya barabara (vikiwemo alama na taa za barabarani). Serikali ya Awamu ya 6, inayoongozwa na Mheshimiwa Rais na Amiri Jeshi Mkuu Dkt. Samia Suluhu Hassan, haitamvumilia mtu yeyote yule atakayebainika kuhusika na uhujumu wa miundombinu. Serikali imewekeza kiwango kikubwa cha fedha kwa ajili ya kujenga na kuendeleza miundombinu mbali mbali kwa ajili ya kuwapatia huduma wananchi.

Nampongeza IGP Camillus Wambura na Jeshi la Polisi kwa ujumla, kwa kuanzisha
Operesheni Maalum ili kupambana kwa weledi na wezi na wahujumu wa miundombinu ya TANESCO, SGR, barabara na miundombinu kwa ujumla.
Ninaagiza Operesheni hii Maalum isiwe tu kwa Mikoa michache, bali iwe endelevu na kwa Mikoa yote Nchi nzima. Watuhumiwa wanaokamatwa Jeshi la Polisi lihakikishe upelelezi unakamilika mapema, na wahusika wanafikishwa katika vyombo vya Sheria, ili Sheria iweze kuchukua mkondo wake.

4) Nalielekeza Jeshi la Polisi kuwa mstali wa mbele, katika kupinga na kupambana
na vitendo vya rushwa kwa vitendo. Na wale wachache ambao sio waaminifu, nawaahidi wananchi kwamba hatua kali zitaendelea kuchukuliwa, kwa mujibu wa
sheria.

5) Nchi yetu imeendelea kupata mvua nyingi katika baadhi ya maeneo nchini, pamoja neema za mvua tunazopata, ikiwemo ustawi wa kilimo na mazingira, na mvua kupita kiasi husababisha kukatika kwa mawasilianao ya barabara na maeneo mengine kujaa maji. Naomba kutoa wito kwa wananchi kuchukua tahadhari kubwa, katika maeneo yenye mikondo ya maji inayokatiza barabarani.

Wazazi na walezi wenzangu tusiache watoto wetu kuvuka pekee yao kwenye maeneo hatarishi ya maji, au kuogelea kwenye madimbwi yanayoweza kusababaisha watoto kupoteza maisha.

Hitimisho
Nitumie fursa hii kuwahakikishia wananchi wote kuwa Nchi yetu iko salama. Ninawaombawatanzania katika umoja wetu tuendelee kumuombea na kumpa ushirikiano Mhe. Rais na Amiri Jeshi Mkuu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika majukumu yake na Uongozi wa Nchi yetu, na hivyo kuifanya Nchi yetu kuendelea kuwa katika hali ya amani na utulivu, na kutufanya sisi sote wananchi kuendelea kushiriki katika shughuli zetu za kiuchumi na kijamii. Amani na usalama wa Nchi yetu ndio msingi wa ustawi wetu kijamii, kiuchumi na hata kisiasa.

Kwa kumalizia, napenda kuwatakia watanzania wote kheri ya sikukuu za Krismas na Mwaka Mpya 2025 wenye mafanikio.

Innocent L. Bashungwa
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI

Previous articleUUNDAJI MAJUKWAA YA UWEZESHAJI WANAWAKE KIUCHUMI UANZE NGAZI YA VIJIJI NA MITAA – WAZIRI DKT. GWAJIMA.
Next articleHAYA HAPA MAGAZETI YA LEO ALHAMISI TAREHE 19,DISEMBA 2024.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here