Na Happiness Shayo – Dar es Salaam
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) amewaasa wahitimu wa Chuo cha Taifa cha Utalii ( NCT) kuleta mageuzi katika utoaji wa huduma bora kwa watalii ili kwenda sambamba na ongezeko la idadi ya watalii nchini ambapo hadi kufikia mwezi Oktoba 2024, idadi ya watalii imefikia asilimia 96% (1,750,198).
Ameyasema hayo leo katika Mahafali ya 22 ya Chuo cha Taifa cha Utalii yaliyofanyika kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam ambapo aliwatunuku vyeti wahitimu 595 katika ngazi za Astashahada na Stashahada katika Fani za Ukarimu, Utalii na Uratibu wa Matukio kwa mwaka 2023/2024.
Aidha, amewapongeza wahitimu hao na kuwaasa kutumia vyema ujuzi walioupata ili kuziba pengo la malalamiko katika eneo la utoaji wa huduma bora kwa wageni.
Katika hatua nyingine, Mhe. Chana amekipongeza Chuo cha Taifa cha Utalii kwa kufundisha lugha ya kichina na kijerumani itakayosaidia kuliteka soko la China na Ujerumani kwa kujiweka tayari kupokea wageni kutoka nchi hizo.
Naye, Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT), Dkt. Florian Mtey aliwapongeza na kuwataka wahitimu hao kwenda kufanya kazi kwa uadilifu huku wakiwa na kiu kubwa ya kuleta maendeleo kwa Taifa.
“Nawapongeza kwa kutumiza vigezo tunaamimi tumewaandaa vya kutosha kwa ajili ya watanzania na kuendeleza mabadiliko ndani na nje ya nchi” alisema Dkt.Mtey.